Rekodi ya Pacome kwa Al Ahly bado inaishi

Muktasari:

  • Pacome alifunga bao dakika ya 90+1 katika sare ya bao 1-1 kwenye mchezo wa Kundi D uliochezwa Desemba 2, 2023 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kiungo wa Yanga, Pacome Zouzoua anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji pekee katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu kuifunga Al Ahly.

Pacome alifunga bao dakika ya 90+1 katika sare ya bao 1-1 kwenye mchezo wa Kundi D uliochezwa Desemba 2, 2023 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Al Ahly ambayo jana Ijumaa ilikata tiketi ya kucheza fainali ya michuano hiyo baada ya kuiondosha TP Mazembe kwa mabao 3-0, imeruhusu bao moja pekee katika kampeni yake msimu huu baada ya kucheza mechi 12 zenye dakika 1080.

Timu hiyo kutoka Misri hadi inatinga fainali tayari imecheza mechi 12, bado mbili kuhitimisha msimu.

Al Ahly iliyoanzia hatua ya pili msimu huu, katika mechi 12 ilizocheza imefunga mabao 19 na kukusanya clean sheet 11.

Mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi ya Mabingwa Afrika wakiwa wamebeba ubingwa mara 11 watacheza fainali dhidi ya Espérance de Tunis ya Tunisia wakihitaji kutetea taji lao na
mchezo wa kwanza utachezwa Mei 18, 2024 nchini Tunisia kisha marudiano Mei 25, 2024 pale Cairo, Misri.

Kwa Al Ahly hiyo itakuwa ni fainali ya 16 ikiwa ndiyo timu iliyocheza fainali nyingi zaidi za michuano hiyo, imeshinda 11 na kupoteza tano.

Msimu uliopita katika mechi 14 za michuano hiyo ambapo ilibeba ubingwa, timu hiyo ilifunga mabao 27 na kuruhusu 10 ikiwa na clean sheet tisa.

MECHI 12 ZA AL AHLY MSIMU HUU
Saint George 0–3 Al Ahly
Al Ahly 4–0 Saint George
Al Ahly 3–0 Medeama
Yanga 1-1 Al Ahly
Al Ahly 0–0 CR Belouizdad
CR Belouizdad 0–0 Al Ahly
Medeama 0–1 Al Ahly
Al Ahly 1-0 Yanga
Simba 0-1 Al Ahly
Al Ahly 2-0 Simba
TP Mazembe 0-0 Al Ahly
Al Ahly 3-0 TP Mazembe