Rekodi ya Mkude yaendelea kuishi

Muktasari:
- Katika mechi hiyo ya juzi, Yanga ilishinda mabao 2-0, yaliyofungwa na Pacome Zouzoua kwa penalti dakika ya 66, baada ya kufanyiwa madhambi eneo la hatari na kipa wa Simba, Moussa Camara, huku Clement Mzize akifunga la pili dakika ya 86.
LICHA ya kiungo wa Yanga, Jonas Mkude kutocheza mechi ya juzi ya Dabi ya Kariakoo dhidi ya Simba, ila nyota huyo ameendeleza rekodi nyingine bora ya kutopoteza mechi yoyote ya dabi hiyo kwenye Ligi Kuu Bara, akiwa amechezea timu hizo zote mbili.
Katika mechi hiyo ya juzi, Yanga ilishinda mabao 2-0, yaliyofungwa na Pacome Zouzoua kwa penalti dakika ya 66, baada ya kufanyiwa madhambi eneo la hatari na kipa wa Simba, Moussa Camara, huku Clement Mzize akifunga la pili dakika ya 86.
Iko hivi, Mkude aliyejiunga na Yanga Julai 12, 2023, baada ya kuachana na Simba aliyoichezea misimu 12, mechi ya juzi ni Dabi ya nane kwake kuzichezea timu hizo mbili, hakuna hata moja aliyopoteza zaidi ya ushindi au sare.
Katika mechi hizo nane, nne aliichezea Simba na kati yake ushindi ni moja, huku nyingine tatu zikiwa sare.
Dabi za sare zilikuwa hivi; Desemba 11, 2021 (0-0), Aprili 30, 2022 (0-0) na Oktoba 23, 2022 (1-1), ambazo zote alianza kikosi cha kwanza, huku mechi ya ushindi ilikuwa ni ya mabao 2-0, dhidi ya Yanga iliyopigwa Aprili 16, 2023, aliyoanzia benchi.
Katika mechi hizo zote akiwa na Simba, Mkude alifundishwa na makocha watatu tofauti akianza na Mhispania, Pablo Franco aliyeongoza dabi mbili, akafuata Juma Mgunda huku wa mwisho na kikosi hicho ni Mbrazili, Roberto Oliveira ‘Robertinho’.
Akiwa na Yanga amehusika katika dabi nne ambazo timu hiyo imeshinda zote, akianza na ushindi mnono wa mabao 5-1, Novemba 5, 2023, ikafuata ya 2-1 iliyochezwa Aprili 20, 2024, kisha bao 1-0, Oktoba 19, 2024 na ya juzi ya ushindi wa 2-0, Juni 25, 2025.
Mbali na hilo, Mkude anayemaliza mkataba wake msimu huu akiwa na kikosi hicho, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji pekee pia ambaye timu zote mbili yaani za Simba na Yanga alizozichezea, zilishinda mabao matano kwenye mechi ya Dabi ya Kariakoo.
Mkude alifanya hivyo wakati Simba ilipoifunga Yanga mabao 5-0, Mei 6, 2012, kisha ikatokea akiichezea pia Yanga msimu wa 2023-2024, ilipoinyuka Simba 5-1, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam Novemba 5, 2023.
Rekodi ya Mkude ilifanywa na nyota wa Denmark, Michael Laudrup aliyezichezea timu mbili hasimu za Hispania, Real Madrid na FC Barcelona.
Laudrup akiwa FC Barcelona, alikiongoza kikosi hicho kushinda mabao 5-0, dhidi ya Real Madrid kwenye Uwanja wa Camp Nou, Januari 8, 1994.
Baada ya kichapo hicho kizito msimu uliofuata, Laudrup akahamia Real Madrid na katika mechi yake ya kwanza tu akiwa na timu hiyo alilipa kisasi na kuishuhudia Madrid ikishinda mabao 5-0, Januari 7, 1995, kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu.
Ushindi huo ukamfanya Laudrup kuingia katika historia ya El Clasico akiwa ndiye mchezaji pekee kushinda kwa mabao matano akizichezea timu zote mbili dhidi ya timu hizo hizo hivyo, kuungana na kiungo, Jonas Mkude aliyezichezea Simba na Yanga.