Redondo awawahi waarabu Dar

KIUNGO mkongwe wa Biashara United, Ramadhani Chombo ‘Redondo’ amerejea mapema kikosini akiuwahi mchezo wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahy Tripoli ya Libya.

Mchezo huo wa mkondo wa kwanza utapigwa leo Ijumaa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na kiungo huyo ameungana na wenzake kwa ajili ya maandalizi baada ya kutoka kumaliza mazishi ya baba yake. Redondo ndiye aliyefunga mabao mawili yaliyoizamisha FC Dikhil ya Djibouti katika mechi ya marudiano iliyopigwa jijini Dar es Salaam na kuivusha timu hiyo kwa jumla ya mabao 3-0 kwani ilishinda ugenini kwa bao 1-0.

Kocha Mkuu wa Biashara, Patrick Odhiambo alisema: “Licha ya matatizo yaliyomkuta ila ni furaha kwetu kurejea kwani tunatambua umuhimu wake kikosini kwetu, kutokana na uzoefu wake aliokuwa nao.”

Akizungumzia na Mwanaspoti juzi mazoezini, Kocha Odhiambo alisema maandalizi yamekamilika na wanajua mchezo huo utakuwa mgumu ila anawajua vizuri wapinzani wake.

“Wakati nipo Gor Mahia (Kenya) nilishakutana nao kwenye mchezo wa kirafiki. Ni timu nzuri yenye matumizi makubwa ya nguvu na akili ila tupo tayari kwa ajili mchezo huo,” alisema.

Meneja wa timu hiyo, Frank Wabare alisema katika mechi yao ya kesho watawakosa wachezaji wanne akiwamo nahodha Abdulmajid Mangalo, Ambrosi Ayoi, Collince Opare na Baron Okechi kwa vile majina yao yalichelewe kuwepo kwenye orodha yao kwa mfumo wa CAF.

“Dirisha la CAF lilikuwa limeshafungwa hivyo hatukuweza kuwasajili kwa wakati, ila waliobaki wote watakuwa sehemu ya mchezo,” alisema.

Biashara United inakutana na Al Ahli Tripoli ya Libya leo kabla ya kurudiana nao wiki ijayo na kama itatoboa hapo itacheza mtoano dhidi ya timu zitakazokwama katika Ligi ya Mabingwa Afrika ili kuwania kutinga makundi.