Ramani Ligi Kuu, Geita Gold , Pamba FC iko hivi

Muktasari:

Pamba FC na Geita Gold zimebakiza mechi moja mkononi baada ya jana Ijumaa kujitupa viwanjani kumenyana na wapinzani wao.

NI vita ya ndugu. Ndivyo unaweza kusema kufuatia mtifuano uliopo kati ya timu za Geita Gold na Pamba katika kumaliza ubishi na kutegua kitendawili cha mashabiki na wadau wa soka katika safari ya kupanda Ligi Kuu msimu ujao.

Hadi sasa tayari kundi A, Mbeya Kwanza ya jijini Mbeya imeshajihakikishia kucheza na Simba na Yanga msimu ujao baada ya kukusanya pointi 38 ikiwa na michezo mitatu mkononi, ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine.

Kimbembe na kasheshe ipo kundi B, ambapo hadi sasa bado kitendawili hakijateguliwa kutokana ushindani ulivyo haswa kwa timu za Geita Gold na Pamba zinavyokimbizana.

Katika kundi hilo, Geita Gold ndio wanaongoza kwa pointi 31 na Pamba wakifuatia kwa alama 30, huku kila timu ikiwa imebakiza mechi mbili kujua hatma yake.

Katika mechi hizo, Geita Gold itaanzia nyumbani leo Ijumaa itakapowaalika Rhino Rangers ambao hawako salama katika kukwepa rungu la kushuka daraja, kisha kuwafuata Fountain Gate huko jijini Dodoma.

Kwa upande wa Pamba wao wanamaliza kazi yao nyumbani kwa mechi zote kuzipiga uwanja wa Nyamagana wakianza na Kitayosce FC leo Ijumaa kisha kuwakaribisha Transit Camp.

Kutokana na mtifuano huo kwa wababe hao wa Kanda ya Ziwa, Mwanaspoti imekuchambulia uwezo na nafasi ya kila timuna historia, lakini ugumu ambao wanaweza kupata na kubaki wakijilaumu mwishoni.


Geita Gold

Timu hii ilianzishwa mwaka 2006 na waliokuwa wafanyakazi wa mgodi wa Geita Gold Mine hususani wale waliokuwa wamecheza mpira kwa miaka ya zamani ‘Vatereni’.

Kipindi hicho walikuwa na viongozi wao, Gurvet Six (Mwenyekiti) Azizi Mwamchori (Makamu Mwenyekiti) Salum Kulunge (Katibu Mkuu) na Mfaume Tunda aliyekuwa Mhasibu.

Kutokana na uhondo waliokuwa wakiupata katika michezo yao ya kujifurahisha na kujitoa jasho baada ya kazi, wakapata wazo la kuisajili kwa ajili ya kushiriki ligi na kuweza kutamburiwa.

Mwaka 2008 wazo liliweza kutekelezwa na kuingia kwenye usajili rasmi kuanza kushiriki ligi daraja la nne, kipindi hicho Geita ikiwa ni wilaya ya Mkoa wa Mwanza.

Timu hiyo iliweza kufanya vizuri na kuchukua ubingwa wa Wilaya na kushiriki ligi ya Mkoa wa Mwanza kabla yam waka 2012 wilaya hiyo kupewa hadhi ya Mkoa na timu hiyo kubaki huko.

Timu hiyo iliendelea na ushiriki wake wa mashindano ambapo msimu wa 2016/17 wakati ikishiriki daraja la kwanza ikiwa kileleni ilikumbana na rungu la kushushwa daraja kwa tuhuma za upangaji matokeo.

Hata hivyo kwa muda wa takribani misimu mitatu timu hiyo ikiwa daraja la kwanza imekuwa ikiishia nafasi ya kucheza play off ya kupanda daraja lakini imekuwa ikizidiwa na timu za Ligi Kuu.

Msimu huu pia imepata bahati ya kuweza kuongoza kundi lake hadi sasa kwa pointi 31, huku ikiwa imebakiza michezo miwili tu kujua hatma yake ambapo mashabiki na wadau mkoani humo wameonesha matumaini makubwa.

Tamu na chungu yake

Geita Gold kwa sasa huenda ikawafuta machozi wadau na mashabiki wake ambao wameisubiri Ligi Kuu kwa takribani misimu mitano bila mafanikio kutokana na mwenendo walionao.

Timu hiyo iwapo itashinda mechi ya leo Ijumaa dhidi ya Rhino Rangers itaendelea kuwapa presha wapinzani, lakini kujiweka pazuri katika kufikia ndoto yake ya kuungana na miamba ya soka nchini, Simba na Yanga.

Pia klabu hiyo imefanikiwa kuwa na kikosi imara haswa wachezaji wenye uwezo na uzoefu, lakini benchi la ufundi lenye makocha safi ambao wana rekodi ya kupandisha timu.

Kocha Fred Felix ‘Minziro’ si jina geni masikioni kutokana na rekodi aliyonayo kwenye ishu ya kupandisha timu Ligi Kuu akifanya hivyo kwa Singida United, KMC na sasa anahitaji kuandika historia nyingine.

Chungu kwa timu hiyo ni pale itakapofanya makosa yoyote aidha kwa kuruhusu sare katika michezo hiyo miwili au kupoteza inaweza kuwapa pigo la kuikosa Ligi Kuu msimu ujao.

Kwa sasa licha ya kwamba Geita Gold inaihofia sana Pamba kuwatiburia, lakini inaweza kujikuta ikiwapa nafasi Kitayosce na Transit Camp ambazo zinakimbiza kimyakimya kwa pointi 27 na mechi mbili mkononi.


Pamba

Klabu hii ni kongwe sana hapa nchini kwani tangu ianzishwe mwaka 1968 imekuwa na historia nyingi na kubwa katika medani za soka na pengine kuzifuata Simba na Yanga.

Timu hiyo ya jijini Mwanza ambayo iliwahi kutwaa ubingwa wa kombe la Muungano mwaka 1990, ilishuka daraja mwaka 1999 na tangu hapo haijawahi tena kucheza ligi kuu.

Msimu wa 2019/2020 iliishia nafasi ya ‘play off’ lakini ilijikuta ikiondoshwa na Kagera Sugar kwa mabao 2-0 na kufifisha ndoto zake za kupanda daraja na leo inapambana kufanya kweli.

Kwa sasa matumaini ya timu hiyo ni kupanda msimu huu, wakipiga hesabu za kushinda michezo miwili iliyobaki, huku wakiiombea mabaya Geita Gold ili kuweza kupanda ligi kuu.


Ugumu wake

Licha ya kuwa na usajili mzuri wa vijana mchanganyiko na benchi imara la ufundi, Pamba ina wakati mgumu kupindua meza kibabe dhidi ya wapinzani wao, Geita Gold.

Vita nzito ni pale itakapopambana kukusanya pointi sita kwa timu ambazo nazo zinapigana kwa nguvu kupanda Ligi Kuu, kwani Transit Camp na Kitayosce nazo zinahesabu kuungana na Simba na Yanga.

Kama haitoshi, iwapo timu hiyo itatoboa kwa ushindi wa mechi hizo, huku Geita Gold nao wakatakata inaweza kuwawia ngumu kuifunga timu ya Ligi Kuu kusaka nafasi ya kupanda daraja kama walivyokwama msimu wa 2019/20.


Wasikie Makocha

Kocha Mkuu wa Geita Gold, Fred Felix ‘Minziro’ anasema mchezo wa leo ni kufa na kupona kuhakikisha wanajiweka pazuri kwenye ndoto zao za kucheza Ligi Kuu msimu ujao.

‘‘Tukifanikiwa pointi tatu za Ijumaa (leo) tutakuwa katika hesabu nzuri za kupanda ligi kuu, hii ndio kiu yetu benchi la ufundi na wana Geita, tumejipanga kimkakati” anasema Minziro.

Naye Kocha wa Pamba, Ulimboka Mwakingwe anasema bado mkakati wao ni uleule kuhakikisha msimu ujao wanashiriki Ligi Kuu na kwamba hesabu zao ni kushinda mechi mbili za mwisho.

“Tunataka alama sita katika mechi hizi za mwisho, hatuangalii wenzetu wamefanya nini au wamekosa nini, vijana kila mmoja anafikiria kupandisha timu hivyo hatuna mzaha kabisa” anasema Mwakingwe.