Rais wa Fifa apiga vitendo vya ubaguzi wa rangi viwanjani

Muktasari:
Huko Uingereza, mashabiki wanajihusisha na tabia ya ubaguzi wa rangi wanakabiliwa na vifungo vya kutohudhuria mechi yoyote uwanjani.
Milan, Italia.Rais wa Shirikisho la Soka duniani (FIFA), Gianni Infantino amesema shirikisho soka la Italia, linatakiwa kuwachukulia hatua kali mashabiki wanaojihusisha na matendo ya ubaguzi wa rangi kama wanayofanya Waingereza.
Katika mchezo wa Jumapili kati ya Atalanta na Fiorentina, uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2, ulikuwa na viashiria vya ubaguzi, ikiwa ni muendelezo wa aina hiyo ya matukio kwenye soka la Italia.
"Hauwezi kuwa na ubaguzi wa rangi katika jamii au katika mpira wa miguu," alisema Infantino. "Huko Italia, hali haijabadilika."
Katika mchezo wa Jumamosi wa Ligi Kuu Italia Serie A, mchezaji wa Fiorentina na timu ya Taifa ya Brazil, Dalbert alimweleza mwamuzi kuwa yeye ndiye aliyelengwa kwa nyimbo za kibaguzi, mchezo huo, ulisimamisha kwa muda.
Tamko la wazi lilipotolewa juu ya tukio hilo kupitia spika kubwa zilizosikika uwanjani hapo, wimbo huo, haukusikika tena na mchezo ukaendelea.
Wiki iliyopita, mashabiki wa Cagliari walishutumiwa kumfanyia ubaguzi wa rangi, mshambuliaji wa zamani wa Manchester United, Romelu Lukaku anayeichezea Inter Milan.
Hiyo ilikuwa ni mara ya tatu kwa Cagliari kutuhumiwa mashabiki wake kuwa na vitendo vichafu vya ubaguzi wa rangi katika miaka miwili iliyopita.
"Ubaguzi unachanganywa na elimu, ulaaniwe," akaongeza Infantino.
"Tunatakiwa kuwabaini wale wanofanya vitendo hivyo na kuwatupa nje ya uwanja. Kama ilivyo nchini England, uhakikisho wa adhabu. Hauwezi kuogopa kulaani wanabaguzi, tunahitaji kupigana nao hadi watakapoacha."