Rais CAF kuzicheki Simba, Yanga Dar

RAIS wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf), Patrice Motsepe na vigogo wengine wakifuatana na mwenyeji wao, Wallace Karia wanaweza kuwa sehemu ya wageni ambao wataungana na Watanzania takribani 60,000 kushuhudia mchezo wa Ngao ya Jamii, leo kwenye Uwanja wa Mkapa utakaozikutanisha Yanga na Simba.

Licha ya kuwa bado hajaithibitishwa lakini taarifa za ndani zinaeleza kuwa Motsepe amekubali mwaliko huo na yupo tayari kushuhudia mchezo huo wa watani wa jadi.

Awali, raia huyo wa Afrika Kusini alitakiwa kuwapo kwenye kilele cha tamasha la Simba Day lakini ilishindikana kutokana na majukumu mazito yaliyokuwa mbele yake kwani alikuwa na mkutano mkuu wa soka Afrika ambao ulifanyika Jumatano jijini Arusha.

Inaelezwa kuwa Simba ilipanga, Agosti 8 kumfanya Motsepe mgeni rasmi ikiwa ni sehemu ya kujibu mapigo ya watani wao ambao walimshusha kocha bora wa Afrika, Pitso Mosimane kwenye kilele cha Siku ya Mwananchi Jumamosi iliyopita, Agosti 6.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa rais huyo wa Caf kuhudhuria mchezo huo wa watani wa jadi ambao umekuwa ukigusa hisia za wengi ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.

Rais aliyepita wa Caf, Ahmad Ahmad aliwahi kuwa mgeni rasmi wa mchezo wa ‘watani wa jadi’ kati ya Yanga na Simba kwenye ligi, Machi 8, 2020.

Kiongozi huyo alifanya ziara ya siku tatu hapa nchini, iliyoanza Machi 7 hadi Machi 10, ambapo katika ziara yake hiyo, Machi 8, alikuwepo kwenye mechi ya watani wa jadi akiwa ni mgeni rasmi.

Ahmad Ahmad alikuwa na utaratibu wa kutembelea mashirikisho mbalimbali ya soka yaliyo chini yake, ambapo mara ya mwisho kuja hapa nchini kabla ya siku hiyo ilikuwa Februari 22, 2018.