Rais CAF: Bao la Aziz KI dhidi ya Mamelodi lilikuwa halali

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Motsepe ameyasema hayo leo akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume wakati akizungumza na Waandishi wa habari mara baada ya kuwasili Visiwani Zanzibar.

Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) Patrice Motsepe amesema bao la kiungo mshambuliaji wa Yanga Stephanie Aziz KI dhidi ya Mamelodi Sundowns lilikuwa halali.

Motsepe ameyasema hayo leo akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume wakati akizungumza na Waandishi wa habari mara baada ya kuwasili Visiwani Zanzibar.

Rais huyo amekuja kuhudhuria fainali za mashindano ya African Schools Football Championship (ASFC) 2024 akipokelewa na mwenyeji wake Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Wallace Karia.

"Niliongeana na Rais Wallace Karia baada ya ile mechi kwamba nilivyotazama mimi marudio niliona ni goli,"amesema Motsepe ambaye amewahi kuwa Rais wa Mamelodi Sundowns.

"Ingawa Rais wa CAF hatakiwi kutoa maoni kuhusu maamuzi ya waamuzi lakini kwangu binafsi nilivyorudia kuangalia lilikuwa ni goli halali lakini naheshimu sana taratibu zote za maamuzi na tunajukumu la kutakiwa kulinda na kuheshimu maamuzi ya waamuzi na mechi kamishna wa michezo kwa afya ya soka letu."

Bao hilo lilizusha utata mkubwa wakati Yanga ikicheza mechi yake ya pili ya mkondo wa pili wa mechi ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns uliopigwa Aprili 5,2024 jijini Pretoria.

Baada ya mwamuzi wa mchezo huo Beida Dahane kutoka Mauritania kukubaliana na maamuzi ya waamuzi wa chumba Cha VAR maamuzi hayo yalikosolewa na mashabiki wengi wakiona hayakuwa maamuzi sahihi.

Aidha Motsepe ameendelea kuzipongeza klabu za Simba na Yanga kwa kuendelea kuwa mfano mzuri wa mashabiki wanaopenda timu zao kwa kujaa vuwanjani zinapocheza.