Pro wa Twiga Stars kaiva
MWANAHAMISI Omary ‘Gaucho’ anayecheza soka la kulipwa nchini Morocco katika klabu ya Shabab Atlas, ameanza mazoezi na timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars, kujiandaa na mashindano ya COSAFA yatakayoanza Septemba 29, nchini Afrika kusini.
Akizungumza baada ya mazoezi katika viwanja vya JK Nyerere jana, Mwanahamisi alisema anaamini kuna kitu atakileta katika kikosi kutokana na alichojifunza tangu aende kucheza soka la kulipwa nchini Morocco.
IMEANDIKWA NA LILIAN MUKULU
“Nimeikuta timu ikiwa na morali ya hali ya juu na wenzangu wanapambana sana, naamini kwa nilichojifunza kwa muda niliokaa Morocco kuna kitu nitakiongeza kwenye timu yetu ya taifa,” alisema Mwanahamisi.Pia kocha mkuu wa Twiga Stars, Bakari Shime alisema maandalizi ya vikosi vyake kuelekea katika michuano ya COSAFA kwa Twiga Stars na kufuzu Kombe la Dunia kwa U20 (Tanzanite) yamekamilika huku akisisitiza kuona mabadiliko ya wachezaji tangu waanze kambi.
Twiga Stars wamepangwa Kundi B kwenye COSAFA sambamba na Zimbabwe, Botswana na Sudani Kusini huku Tanzanite wakitarajia kucheza mchezo wao kwa kwanza wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Eritrea Septemba 26 mwaka.