Prisons yapata mtathmini mchezo

KLABU ya Tanzania Prisons ipo mbioni kumtangaza Faraji Muya 'Enzo' kuwa mtathmini mchezo (Video Analyst) kwa njia ili kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri kwenye Ligi Kuu.

Enzo alikuwa meneja wa klabu ya KMC iliyopo Ligi Kuu na baadae alisomea ukocha wa utimamu wa mwili pamoja na utathmini mchezo kwa ajili ya kuongeza fani katika soka.

Habari ambazo Mwanaspoti linalo ni kwamba Enzo ameshaanza kazi na alisafiri na timu hiyo hadi katika mchezo wao dhidi Ihefu uliomalizika kwa suluhu (0-0) na Mashujaa ambapo walishinda 2-0 mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.

Inaelezwa mabosi wa Tanzania Prisons wanampa kazi hiyo Enzo kwa lengo la kuisuka timu hiyo kuanzia kwenye dirisha dogo la usajili ili kushusha watu wa kazi.

"Kweli yupo huku na sisi na tulisafiri nae, mabosi wamempa cheo hicho kwa lengo la kuhakikisha tunapata wachezaji wazuri kwa sababu na yeye ana uzoefu na soka la hapa nyumbani,"kilisema chanzo kutoka ndani ya timu hiyo na kuongeza;

"Tunamsubili mkuu wetu tu kwa sababu hakuwa ofisini na hizi ni timu za jeshi kwahiyo kuna vitu hauwezi kutangaza hadi vitangazwe."

Enzo alianza kuonekana wakiwa jukwaani jijini Mbeya timu hiyo ilipocheza na Dodoma Jiji  akiwa na kocha mpya wa timu hiyo , Hamad Ally ambaye amekaa benchi kwenye mechi mbili dhidi ya Ihefu 0-0 na Mashujaa 2-0.

Wawili hao pia waliwahi kufanya kazi kwa pamoja wakati wakiwa wanaitumikia Kmc ya jijini Dar es Salaam.

Enzo pia aliwahi kuwa meneja kwenye timu ya Mbao FC ambayo ilicheza fainali ya kombe la Fa dhidi ya Simba (2017) na ilipoteza kwa kufungwa 2-1.