Prisons: Tukutane msimu ujao muone!

Muktasari:
- Josiah ambaye ilikuwa msimu wake wa kwanza kufundisha timu ya Ligi Kuu, amesubiri hadi mchezo wa mwisho wa play off dhidi ya Fountain Gate na kujihakikishia kubaki salama katika Ligi Kuu msimu ujao.
‘TUKUTANE msimu ujao’. Ni kauli ya kocha mkuu wa Tanzania Prisons, Aman Josiah akielezea furaha yake kuibakiza timu hiyo Ligi Kuu, akibainisha kuwa nyota wake na uongozi umempa heshima.
Josiah ambaye ilikuwa msimu wake wa kwanza kufundisha timu ya Ligi Kuu, amesubiri hadi mchezo wa mwisho wa play off dhidi ya Fountain Gate na kujihakikishia kubaki salama katika Ligi Kuu msimu ujao.
Maafande hao katika Ligi Kuu walimaliza kwenye nafasi ya 13 kwa pointi 31 na kuangukia mchujo (playoffs) dhidi ya Fountain Gate na katika mechi mbili wameshinda kwa jumla ya mabao 4-2 na kukwepa kushuka daraja.
Matokeo hayo yaliifanya timu hiyo ya Jeshi la Magereza kubaki Ligi Kuu, huku Fountain Gate ikisubiri kuvaana na Stand United ya Championship ili kujiuliza kubaki au kushuka daraja msimu ujao.
Josiah amesema haikuwa kazi raihisi lakini kwa uongozi wa timu hiyo na wachezaji kwa ujumla wamempa heshima kutokana na ushirikiano walioonyesha kwa muda alioaminiwa kufundisha timu hiyo.
Amesema kwa sasa wanaenda kujipanga upya kwa ajili ya msimu ujao kuhakikisha makosa yaliyoonekana wanayafanyia kazi ili warejee na nguvu mpya ndani na nje ya uwanja.
“Niwapongeze wachezaji kwa kuniheshimisha, uongozi ulinipa ushirikiano na kufanikiwa kubaki salama Ligi Kuu, haikuwa kazi raihisi lakini kila mmoja amepambana kwa nafasi yake na kuweza kufikia malengo,” alisema Josiah.
Alisema pamoja na ugeni aliokuwa nao katika kazi hiyo, mapambano yamempa nguvu na uzoefu hivyo anaamini kwa msimu ujao anaweza kufanya makubwa zaidi akiwaomba mashabiki kuendelea kutoa ushirikiano kwa timu hiyo.