Prisons: Simba? Tukutane Sokoine

BAADA ya kumaliza dakika 180 bila kuonja ushindi, Tanzania Prisons imesema sasa inarejea Sokoine na yeyote aje ikitamba kuinyoosha Simba na kuianza rasmi Ligi Kuu.

Maafande hao walianzia ugenini mechi tatu na kuambulia pointi moja dhidi ya Singida Fountain Gate na kupoteza mbili mbele ya Azam FC na Tabora United ikiruhusu mabao 3-1 kila mechi.

Kwa sasa Wajelajela hao wanatarajia kurejea uwanja wa nyumbani dhidi ya Simba ikiwa ni mechi yao ya kwanza mbele ya mashabiki, mchezo utakaopigwa Oktoba 5.

Kocha mkuu wa timu hiyo, Fred Felix ‘Minziro’ alisema pamoja na kutofikia malengo yao, lakini vijana walipambana ila matokeo ya mpira yalikuwa hivyo na sasa wanaenda kuanza kazi na Simba.

Alisema kawaida ya michezo ya ugenini inakuwa na ugumu wake akieleza kuwa hata mchezo ujao dhidi ya Wekundu utakuwa mgumu kutokana na wapinzani hao kuwa na kikosi bora na mashabiki wengi kila wanapokuwa.

“Tunarudi nyumbani, iwe jua iwe mvua kitaeleweka hukohuko, tunafahamu kukutana na timu kubwa kama hizo ushindani unakuwa mkali kutokana na mashabiki wao kuwa wengi, lakini tunaenda kuanza rasmi ligi,” alisema Minziro na kuongeza;

“Zaidi ni kuwaandaa wachezaji kisaikolojia na kiufundi kuhakikisha hawatoki mchezoni, lazima wajue kwamba huu ni mpira na matokeo yapo, makosa yaliyoonekana tutayafanyia kazi.”

Kocha huyo aliongeza bado upungufu ni eneo la ushambuliaji kutotumia vyema nafasi wanazopata na pia kuruhusu mabao sita kwenye mechi mbili mfululizo siyo afya sana kwao na hakutarajia.

“Matokeo bado hayajawa mazuri kwa sababu raha ya mpira ni bao na ushindi, lakini naamini tutaimarika.”