Prisons Queens waisikilizia TFF

Muktasari:
- Prisons Queens ambayo ilianzishwa mapema mwaka huu ndio bingwa wa Ligi ya Wanawake Mkoa wa Mbeya, ambapo ilishiriki Ligi ya Mabingwa wa Mikoa kwa soka la Wanawake na kuishia nafasi ya tatu.
BAADA ya kukabidhiwa majukumu kuiongoza Prisons Queens, Kocha Mkuu Shaban Mtupa amesema anahitaji kuweka historia kwa timu hiyo kucheza Ligi Kuu misimu miwili ijayo, huku akilisikilizia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Prisons Queens ambayo ilianzishwa mapema mwaka huu ndio bingwa wa Ligi ya Wanawake Mkoa wa Mbeya, ambapo ilishiriki Ligi ya Mabingwa wa Mikoa kwa soka la Wanawake na kuishia nafasi ya tatu.
Katika ligi hiyo iliyofanyika jijini Dodoma, Maendeleo Queens ndio walitwaa ubingwa na kupanda daraja la kwanza, huku Bunda Girls ikishika nafasi ya pili na Wajelajela hao kumaliza nafasi ya tatu.
Hata hivyo, ilielezwa kuwa huenda timu hiyo ya jijini Mbeya ikapata ‘mchekea’ kupanda daraja la kwanza, ambapo hadi sasa bado hakijaeleweka huku wakiendelea na maandalizi.
Akizungumza baada ya mchezo wao wa kirafiki dhidi ya Inyala Queens walioshinda mabao 13-0, Mtupa alisema anaona mabadiliko mazuri kikosini, akieleza kuwa ndoto zao ni kucheza Ligi Kuu.
Alisema wakati wakiendelea na maandalizi yao, sikio lao lipo TFF iwapo itawapa nafasi ya kushiriki daraja la Kwanza ili kuweza kuwarahisishia safari yao ya matumaini.
“Nimeona mabadiliko mazuri japokuwa tunahitaji mechi nyingi za kujipima nguvu zikiwamo za madaraja ya juu ili kutupa muelekeo mzuri kabla ya kuanza msimu ujao.”
“Tuliambiwa na TFF kwamba tuendelee kujiandaa wakati wakiangalia uwezekano, kimsingi sisi tuko tayari kwakuwa vijana kila siku wanaonesha ubora uwanjani,” alisema Mtupa.
Alipotafutwa Afisa Habari wa Shirikisho la Soka, Cliford Ndimbo licha ya kutojibu moja kwa moja, aliomba kupewa nafasi kufuatilia usahihi wa taarifa hiyo.
“Nani aliwaambia? Najaribu kufikia sielewi ila nipe muda nifuatilie kwanza nijue ikoje hiyo,” alijibu Ndimbo kwa ufupi alipoulizwa hatma ya timu hiyo kupanda daraja.