Prisons hakuna kulala, nyota waahidi makubwa

Thursday May 12 2022
prisons pic
By Saddam Sadick

Mbeya. Baada ya kuondoka na alama moja katika mechi iliyopita dhidi ya Yanga, Tanzania Prisons imeendelea na mazoezi yao kujiandaa dhidi ya Kagera Sugar huku nyota wa timu hiyo wakisisitiza kuwa hakuna kushuka daraja.

Prisons iliambulia suluhu dhidi ya vinara wa Ligi Kuu katika mchezo uliopigwa uwanja wa Taifa Dar es Salaam na sasa wanajiandaa tena kuwavaa Kagera Sugar mechi itakayochezwa Sokoine Mei 16.

Hadi sasa Wajelajela hao wamekusanya pointi 23 na kuwa nafasi ya 14 ambapo wanahitaji ushindi zaidi ili kujiweka pazuri au kujihakikishia kubaki Ligi Kuu msimu ujao.

Wakizungumza leo Alhamisi wakati wa mazoezi yao yaliyofanyika uwanja wa Magereza jijini hapa, wamesema kwa sasa ari na morari ni kubwa kikosini na kwamba wanaendelea kupambana kusaka ushindi kila mechi ili kujihakikishia kubaki kwenye Ligi.

Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Shaban Mtupa amesema kwa sasa akili zao zipo katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar kuhakikisha wanapata alama tatu ambazo zitawaweka pazuri kwenye msimamo.

"Vijana wako vizuri mazoezini tunajiandaa na Kagera Sugar tukiamini siyo mechi nyepesi, bado tuna kazi ngumu na hatujabweteka kila mchezo kwetu ni vita ya pointi tatu" amesema Mtupa.

Advertisement

Naye Kipa wa timu hiyo, Hussein Abel amesema mechi sita alizodaka hadi sasa ikiwamo ya Yanga, zimempa kujiamini lakini kuendeleza ubora wake ili kuisaidia timu kubaki kwenye Ligi huku akiwatoa hofu mashabiki kuwa Prisons itafanya vizuri mechi zilizobaki.

"Mechi hizi zimenipa kujiamini niwaombe wenzangu kuongeza juhudi lakini mashabiki nao waendelee kutusapoti, tutaendelea kupambana na timu haishuki daraja " amesema Abel.

Nahodha wa timu hiyo, Benjamin Asukile amesema wanajua ugumu wa mechi yao ijayo na Kagera Sugar kwani wapinzani wametoka kupoteza mechi zao sawa na wao kwani walihitaji ushindi dhidi ya Yanga lakini waliishia alama moja hivyo wanasubiri mchezo huo kulipiza walichopoteza.

"Wamepoteza mechi yao kama sisi ambao tulipoteza kwa Mbeya Kwanza lakini suluhu na Yanga, matokeo hayo si mazuri kwetu hivyo tunasubiri Kagera Sugar kufidia kile tulichopoteza" amesema Asukile.

Advertisement