Prince Dube, Azam sasa kumekucha TFF

Muktasari:

  • Mwanaspoti awali liliripoti kwamba Prince Dube ameukana mkataba wake na Azam FC unaomalizika 2026 na akaondoka Chamanzi. Staa huyo alikwenda kushtaki kwenye Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) na kesi yake imepangwa kuanza kusikilizwa kesho, Aprili 18.

Picha la Azam FC na Prince Dube limeanza upya na kuanzia kesho yatafichuka mengi pande hizo mbili zitakapokutana uso kwa uso kwa mara nyingine.

Mwanaspoti awali liliripoti kwamba Prince Dube ameukana mkataba wake na Azam FC unaomalizika 2026 na akaondoka Chamanzi. Staa huyo alikwenda kushtaki kwenye Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) na kesi yake imepangwa kuanza kusikilizwa kesho, Aprili 18.

Dube alipeleka kesi hiyo TFF na Mwanaspoti liliripoti kwa mara ya kwanza taarifa hiyo pamoja na maisha ya kifahari anayoishi kwa sasa maeneo ya Salasala jijini Dar es Salaam chini ya ulinzi mkali wa mabaunsa wanaopeana zamu.

Katika kesi yake ya msingi, Dube anasema mkataba wake na Azam FC utaisha Juni 2024 siyo Juni 2026 kama inavyodai Azam FC.

Haijajulikana Dube atawakilishwa na nani kwenye kesi hiyo, lakini taarifa za ndani kutoka Azam FC zinasema klabu hiyo imeajiri mwanasheria kutoka Ureno kuiwakilisha.

Staa huyo amekuwa akihusishwa na klabu kadhaa ikiwemo Al Hilal na Simba ambazo Azam imezichomolea ofa zao. Inaelezwa kwamba watu wa karibu na Yanga wamemhifadhi mchezaji huyo Dar es Salaam na wameshampa ofa ya miaka miwili, wamemnunulia thamani za ndani za Sh30 milioni na ulinzi wa saa 24 ambao alienda nao hadi TFF na hata viwanjani.

Yanga licha ya kwamba hawajaenda rasmi Azam FC, lakini watu walio karibu na timu hiyo yenye maskani yake Jangwani  wamemuongezea ulinzi huo kwani hawataki abughudhiwe na wapinzani wao hususan Simba ambao wanamtaka kwa udi na uvumba.   

Kwenye taarifa ya Azam waliyoitoa kuhusu Dube kuomba kuvunja mkataba, Azam FC walisema mkataba wao na mchezaji huyo utaisha 2026 na Mwanaspoti limeambiwa wanamuuza SH700 milioni wakati alishawaomba awarudishie milioni 500 walizompa ili wakati waachane kiroho safi.

Dube alijiunga na Azam FC Agosti 2020 kwa kusaini mkataba wa miaka miwili hadi 2022. Mwaka mmoja baadaye, 2021, alisaini nyongeza ya mkataba hadi 2024.

Huo ndiyo mkataba ambao Dube anadai kuutambua. Lakini Azam FC wanadai kwamba mwaka 2023 raia huyo wa Zimbabwe alisaini tena mkataba hadi 2026. Huo ndiyo mkataba ambao anaukana.

Wakala wa Prince Dube, Gerge Deda kutoka Zimbabwe amekuwa akikwepa kufafanua sakata la mteja wake.

Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Said Soud, amethibitisha kwamba kesho wana kikao cha kujadili ambapo kwa kawaida vikao huanza saa 4:00 asubuhi, huku akibainisha kwamba kuna mambo mengi wanajadili na sio ishu ya Dube pekee.

"Inategemea ni ishu gani tunaikuta mezani siku husika ya kikao. Kuna wakati zinakuwepo kesi zaidi ya 10 tunachambua moja baada ya nyingine, hivyo sijui itakuwa ya nani na nani," amesema Soud.

Akizungumzia suala hilo, wakili wa kujitegemea Aloyce Komba amesema suala la mkataba ni siri kati ya mchezaji na klabu ingawa mikataba yote inapaswa kuwasilishwa kwenye Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji iliyopo chini ya TFF.

"Kwenye kanuni za Fifa inazungumzwa mchezaji ana haki ya kujieleza kutokana na makubaliano aliyoingia ingawa kama kwenye makubaliano lazima yawe na dokumenti zinazoonyesha na sio kuangalia suala la mkataba wa awali 'pre contract' bila ya maandishi.

"Kama mchezaji anasema mkataba wake unaisha mwishoni wa msimu ila klabu yake inasema hadi 2026 ni lazima uwe umesajiliwa rasmi ili kuondoa mgongano wa kimaslahi baina yao, hata hivyo Kamati ya TFF ndio inayojua ukweli wa hilo," anasema.

Kwa upande wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Kamati ya Katiba ya Hadhi, Sheria na Hadhi za Uanachama wa Shirikisho la mpira wa Miguu, Eliud Mvela alisema: "Hilo sio jambo gumu, ili mkataba wako uongezwe ni lazima usajiliwe TFF ili kulinda usalama wa mchezaji labda kama kuwe na kipengele cha kuvunja mkata kwa mfano atakapotakiwa na timu nyingine anashauriwa kuondoka japo kwa makubaliano."

Kesi ya Dube inataka kufanana na kesi kadhaa za wachezaji wa ligi ya Tanzania.

BERNARD MORRISON VS YANGA (2020)

Mchezaji huyo raia wa Ghana alijiunga na Yanga Januari 2020 akisaini mkataba wa miezi sita.

Baada ya miezi michache Yanga wakatoa picha za mchezaji huyo akiwa na kiongozi wa timu hiyo, Hersi Said wakisema amesaini nyongeza ya mkataba.

Lakini mwisho wa msimu, Bernard Morrison akasema hakusaini nyongeza ya mkataba na hata zile picha aliombwa apige ili kutuliza upepo.

Wakati sakata likiendelea, Morrison akatambulishwa na Simba.

Kesi ikaenda TFF na Yanga wakashindwa. Wakakata rufaa kwenye Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo ya Fifa, ambako pia walishindwa na Morrison akajiunga na Simba kwa ajili ya msimu wa 2020/21.

RAMADHAN SINGANO VS SIMBA

Mwaka 2015 chipukizi wa Simba kutoka timu ya vijana, Ramadhani Singano alikana mkataba wake na klabu hiyo akisema haukuwa mrefu kama Simba walivyodai.

Singano alisema mkataba wake na klabu hiyo ulikuwa wa miaka miwili na ndiyo ulikuwa unaisha baada ya msimu wa 2014/15, lakini Simba walisema alisaini miaka mitatu na mkataba ulitakiwa kuisha baada ya msimu wa 2015/16.

Kesi ikaenda TFF na kupigwa sarakasi ya karne. Kesi ya msingi ılıtupwa na kuibuliwa kesi mpya ya Simba kutotimiza vipengele vya mkataba ikiwemo bima ya afya na makazi.

Hata hivyo, Simba walidai walikuwa wakimpa pesa hizo mchezaji huyo kwenye jumuisho la pamoja la mshahara wake. Mchezaji alikana hilo na akataka Simba wathibitishe kwa stakabadhi za malipo.

Simba wakasema uangaliwe mshahara wa mchezaji huyo kwenye mkataba na iangaliwe pesa aliyokuwa akilipwa kama mshahara.

Ukweli ilionekana alikuwa akilipwa pesa nyingi kuliko mshahara wake, lakini ongezeko halikuwa na maelezo ya maandishi.

Simba wakadai hilo ongezeko ndiyo fedha za makazi na afya, lakini walisema kwa mdomo tu kamati ikatupilia mbali kesi na kumtangaza Ramadhan Simba kuwa mchezaji huru akajiunga na Azam FC.

ATHUMAN IDD CHUJI VS SIMBA 2007

Hii ni moja ya kesi ambazo hazikuwahi kupata majibu hadi leo.

Chuji alikuwa mchezaji wa Simba tangu 2005 akitokea Polisi Dodoma.

Mwaka 2007 akasema mkataba wake na Simba ulikwisha na akasaini Yanga. Simba wakadai mkataba haukuwa umeisha hivyo kesi ikaenda TFF.

Simba wakatoa mkataba na Chuji akatoka mkataba wake. Chuji akaikana sahihi iliyokuwa kwenye mkataba walioutoa Simba.

Ikabidi mikataba yote ipelekwe kitengo maalumu cha Polisi cha kutambua sahihi za watu.

Majibu hayakuwahi kutoka hadi TFF ilipoamua kuuvunja mkataba na kumuacha mchezaji huyo huru akajiunga na Yanga. Sasa ni zamu ya Prince Dube. Endelea kufuatilia Mwanaspoti tutakupa kila kinachoendelea.