Presha ya wanachama vigogo Yanga wakimbia jengo lao

Muktasari:

Kikao hicho cha viongozi wa kamati ya utendaji kimeitishwa kwa dharura kubadili hatua ya mmoja wa wadhamini wao kampuni ya GSM kutangaza kusitisha kufanya majukumu ambayo yapo nje ya mkataba wa pande hizo mbili.

Dar es Salaam. Presha ya kumuondoa kwa mmoja wa wadhamini wa Yanga kampuni GSM kumeibua jipya baada ya viongozi wa klabu hiyo kuamua kukimbia jengo lao kwa muda.

GSM ambao ni wadhamini wa Yanga jana Machi 25, 2020 walisitisha kutekeleza majukumu ya nje ya mkataba wao na klabu hiyo kongwe kwa sababu iliyotajwa kwamba baadhi ya viongozi wa timu hiyo kuona wanaingiliwa majukumu yao na kampuni hiyo.

Majukumu ambayo GSM waliyasitisha ni pamoja na kufanya usajili, kulipa wachezaji mishahara na posho,kulipa gharama za kambi na hata mazoezi.

Hatua hiyo ikaifanya Yanga kuitisha kikao cha dharura cha kamati ya utendaji ambacho kinafanyika mchana huu huku tofauti na kawaida yao safari hii wakakifanyia nje ya makao makuu ya klabu hiyo.

Viongozi hao taarifa za uhakika ambazo zimepatikana ni kwamba kikao hicho sasa kitafanyika kwa siri maeneo ya masaki kikipangwa kuanza saa nane mchana.

Imeelezwa kwamba kikao hicho kitafanyika katika moja ya ofisi ya kigogo mmoja wa juu wa klabu hiyo ambaye amejitolea ofisi yake hiyo binafsi kubeba jukumu hilo.

Aidha imeelezwa kwamba sababu kubwa ya maamuzi hayo ni kutokana na baadhi ya wajumbe kuhofia usalama wao kutoka kwa wanachama wao ambao wameonyesha kuchukizwa na hatua ya GSM kujitoa huku sababu ikitajwa kwamba chanzo ni malalamiko ya baadhi ya viongozi wao.

Tangu uongozi wa Mwenyekiti Dk Mshindo Msolla uingie madarakani vikao hivyo vingi vimekuwa vikifanyika makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo mitaa ya Twiga na Jangwani.