Pogba asimulia alivyoingia kwenye uislamu

Muktasari:
Pogba, ambaye kwa sasa anahusishwa na mpango wa kutimkia Real Madrid, anakosakwa mchana usiku akakipige kwenye kikosi cha Kocha Zinedine Zidane, anasema dini hiyo imembadili sana na kumfanya kuwa mpenda amani zaidi.
PARIS,UFARANSA .PAUL Pogba anasema amejiuliza maswali mengi kabla ya kuamua kuingia kwenye dini ya Kiislamu ambayo anasema imempa amani kubwa ndani ya moyo.
Kiungo huyo wa Manchester United, ambaye mwezi uliopita alikwenda Umra huko Mecca katika kipindi cha Mfungo wa Mwezi wa Ramadhani, wakati anakuwa hakukuzwa kwa maadili ya Kiislamu, licha ya kwamba mama yake, Yeo Moriba alikuwa ni muumini wa dini hiyo.
Lakini baada ya kukumbana na vikwazo vingi, Pogba aliamua kufanya uchunguzi wake wa kina kuhusu dini hiyo na kuamua kuungana na marafiki zake kadhaa ambao walikuwa wameingia kwenye imani ya dini ya Kiislamu.
Tangu wakati huo supastaa huyo wa kimataifa wa Ufaransa, ambaye aliwahi kuvunja rekodi ya dunia kwenye uhamisho alipotua Man United kwa ada ya Pauni 89 milioni akitokea Juventus, amekuwa muumini thabiti wa dini ya Kiislamu na mara kadhaa amekuwa akihudhuria ibada ya Umra na hija huko Mecca.
Pogba, ambaye kwa sasa anahusishwa na mpango wa kutimkia Real Madrid, anakosakwa mchana usiku akakipige kwenye kikosi cha Kocha Zinedine Zidane, anasema dini hiyo imembadili sana na kumfanya kuwa mpenda amani zaidi.
Staa huyo wa zamani wa Juventus anasema alikuwa mkorofi sana, lakini anashukuru kuingia kwenye Uislamu kumemfanya abadilike kitabia na kuwa mtu safi na mnyenyekevu.
Katika mahojiano yake na The Times, Pogba alizungumzia kuhusu Uislamu kwa upande wake na kusema: “Ni kila kitu. Hilo ndilo linalonifanya nishukuru kwa kila jambo.
“Imenifanya nibadilike, kufahamu mambo mengi kwenye maisha. Nadhani imenifanya kuwa na amani zaidi moyoni.
“Yalikuwa mabadiliko mazuri katika maisha yangu kwa sababu sikuzaliwa Muislamu, licha ya kwamba mama yangu alikuwa Muislamu. Hivyo ndivyo nilivyokuzwa, kumheshimu kila mtu.
“Uislamu haupo kama watu wengi wanavyouona, ugaidi … kile kinachozungumzwa kwenye vyombo vya habari ni kitu tofauti kabisa. Uislamu ni kitu kimoja kizuri sana.
“Ukiufahamu vizuri. Basi utagundua kila mtu ana uhusiano na Uislamu.”
Baada ya kumalizika kwa msimu uliopita ambapo kikosi chake cha Man United kilishika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu England na kushindwa kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, Pogba na Mfaransa mwenzake, beki wa Chelsea, Kurt Zouma waliamua kwenda Mecca kufanya ibada katika kipindi cha Mfungo wa Mwezi wa Ramadhan.
Mara moja kwa mwaka, zaidi ya Waislamu milioni mbili wamekuwa wakisafiri kutoka pande zote za dunia hii kwenda hija, huko Saudi Arabia kufanya ibada muhimu ambayo ni moja kati ya nguzo kuu za Kiislamu.
Staa huyo aliingia kwenye Uislamu akiwa na umri unaoanzia miaka 20 na alipoulizwa kwanini amefanya hivyo, Pogba, ambaye hanywi pombe na ambaye amepata mtoto hivi karibuni na mchumba wake, mrembo Maria Salaues, alisema: “Kwa sababu nina marafiki wengi sana Waislamu. Siku zote tumekuwa tukizungumza hilo.
“Nilijiuliza maswali mengi sana, kisha nikaanza kufanya utafiti wangu. Niliswali siku moja na marafiki zangu na hapo nikagundua kitu tofauti. Nilijisikia vizuri sana.
“Tangu siku hiyo nimekuwa muumini wa dini ya Kiislamu. Unapaswa kuswali sara tano kwa siku, hiyo ni moja ya nguzo ya Uislamu. Hicho ndicho unachotakiwa kufanya.
“Maana kubwa ya kufanya hivyo ni kumwomba msamaha Mwenyezi Mungu na kushukuru kwa kila ulichonacho, kama vile afya na mengineyo.
“Ni dini iliyofungua akili na kunifanya hivi nilivyo kwa sasa, nimekuwa mtu safi. Unafikiria zaidi kuhusu maisha baada ya uhai. Haya maisha yana majaribu mengi. Nimekuwa na wewe hapa, hata kama si Muislamu, lakini nakutambua ni mwanadamu mwenzangu, sipaswi kukubagua kwa dini yako, kwa rangi yako au kwa kitu chochote kile.
“Ndio hivyo ulivyo Uislamu, unaheshimu utu na kila kitu.”