Pluijm apangua wanne akiivaa Geita Gold, Ajibu yupo

KOCHA Mkuu wa Singida Big Stars, Hans Van De Pluijm amepangua nyota wanne katika kikosi chake kinachoivaa Geita Gold leo muda mfupi ujao kuanzia saa 10:00 jioni katika Uwanja wa Liti mkoani Singida, huku nyota mpya wa timu hiyo, Ibrahim Ajibu akijumuishwa kikosini.

Nyota wanne ambao wamepanguliwa ni beki wa kulia, Juma Abdul, beki wa kushoto, Shafiq Batambuze, kiungo, Said Ndemla na mshambuliaji, Nicolas Gyan ambao walianza katika mchezo uliopita ugenini dhidi ya Dodoma Jiji na kupata ushindi wa bao 1-0.

Kocha huyo amewaanzisha beki wa kulia, Paul Godfrey ‘Boxer’, kiungo, Yusuph Kagoma, winga, Deus Kaseka na Rodrigo Fegu kuziba nafasi za nyota hao.

Singida Big Stars inakamata nafasi ya nne kwenye ligi ikishinda mechi 10, sare nne na kupoteza nne, ikifunga mabao 20 na kuruhusu 14 ikivuna pointi 34, huku Geita Gold ikiwa katika nafasi ya saba, ikishinda michezo mitano, sare tisa na kupoteza minne, ikifunga mabao 2o na kuruhusu 24 ikivuna pointi 24.

Kikosi cha Singida BS kinachoanza ni kipa, Benedict Haule, mabeki wa pembeni ni Paul Godfrey na Nickson Kibabage, mabeki wa kati, Paschal Wawa na Biemes Carno, viungo ni Yusuph Kagoma, Aziz Andambwile na Bruno Gomes, mawinga ni Deus Kaseke na Rodrigo Fegu huku mshambuliaji akiwa ni Meddie Kagere.

Wanaoanzia benchi ni Abubakar Khomeiny, Abdulmajid Mangalo, Dario Frederico, Yasin Mustapha, Said Ndemla, Frank Zakaria, Robin Sanga, Ibrahim Ajibu na Nassoro Saadun.

Kwa upande wa Geita Gold, kocha, Fredy Felix ‘Minziro’ amepangua wachezaji wawili katika kikosi chake cha leo akiwapumzisha mabeki wake wawili wa pembeni walioanza katika mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar timu hiyo ikilazimishwa sare ya 2-2.

Waliopanguliwa ni beki wa kulia, George Wawa na beki wa kushoto, Yahya Mbegu ambaye hajajumuishwa kabisa katika kikosi cha leo huku akihusishwa na tetesi za kuondoka klabuni hapo ikiwa ni miezi sita tu tangua jiunge kutoka Polisi Tanzania.

Kikosi kinachoanza cha Geita Gold ni Sebusebu Samson, Haruna Shamte, Amosi Kadikilo, Kelvin Yondani, Hussein Kazi, Kelvin Nashon, Deusdedith Okoyo, Jofrey Manyasi, Juma Luizio, Dany Lyanga na Alphonce Mbindo.

Kikosi cha akiba ni Arakaza McAthur, George Wawa, Jonathan Mwaibindi, Oscar Masai, Shinobu Sakai, Ramadhan Chombo, Offen Chikola na Edmund John.