Pluijm ampa tuzo Mayele

Muktasari:

  • Kauli ya Pluijm inajiri siku chache tu tangu nyota huyo afunge bao katika ushindi wa 1-0 na kuitoa Singida kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), iliyopigwa Uwanja wa Liti Singida.

KOCHA Mkuu wa Singida Big Stars, Hans Van De Pluijm amesema licha ya Ligi Kuu Bara kubakisha michezo miwili kumaliza msimu ila nyota wake bora hadi sasa ni mshambuliaji na kinara wa mabao wa Yanga, Fiston Mayele.

Kauli ya Pluijm inajiri siku chache tu tangu nyota huyo afunge bao katika ushindi wa 1-0 na kuitoa Singida kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), iliyopigwa Uwanja wa Liti Singida.

"Ukiniuliza mimi nitakwambia anastahili mchezaji bora wa msimu kwani anajua kufunga, ana spidi na anaweza kujiweka katika mazingira mazuri uwanjani, hivyo kwangu binafsi ni mshambuliaji aliyekamilika," alisema.

Pluijm aliongeza hata mafanikio makubwa ambayo Yanga imefikia msimu huu ni jitihada kubwa za mshambuliaji huyo kwa sababu licha ya viongozi kufanya kazi yao nje ya uwanja ila pia Mayele amehusika kwa kiasi kikubwa.

"Viongozi hawaepuki pongezi zao kwa jinsi ambavyo wamekuwa mstari wa mbele kuiandaa timu na kuiweka katika mazingira mazuri lakini Mayele anastahili heshima zake licha ya kwamba ni ushirikiano na wachezaji wenzake."
Msimu huu Mayele amekuwa mwiba kwa Singida kwani licha ya kuitoa kwenye nusu fainali ya ASFC ila aliifunga mabao matatu

'Hat-Trick' katika ushindi wa timu hiyo wa 4-1 Novemba 17, mwaka jana Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Katika michezo yote miwili ya Ligi Kuu Bara ambayo Pluijm ameingoza Singida haijawahi kuifunga Yanga kwani hata mchezo wa mzunguko wa pili uliopigwa Uwanja wa Liti Singida Mei 4, mwaka huu alifungwa  mabao 2-0.

Mayele anaongoza kwa ufungaji bora hadi sasa katika Ligi Kuu Bara kwani amefunga mabao 16 huku akiiwezesha pia Yanga kutinga hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo itacheza na USM Alger ya Algeria Mei 28.