Phiri ataja sababu kusaini Simba

STRAIKA wa Zanaco, Moses Phiri ameitaja kwa mara nyingine klabu ya Simba akisema ni timu kubwa na hakuna mchezaji anayeweza kuigomea kucheza.

Phiri mwisho wa msimu huu amemaliza mkataba wake na Zanaco na tayari ameshamalizana na Simba akisaini mkataba wa miaka miwili kuja kwa wekundu hao ambao wameanza kukusanya mastaa wapya kwa ajili ya msimu ujao.

Mwanaspoti lilimtafuta Phiri ambaye ametambulishwa jana na Simba akisema anavutiwa na mafanikio ya timu hiyo anga ya kimataifa.

“Nahitaji kubadilisha mazingira ya maisha kwa kupata changamoto mpya. Simba ni moja ya klabu kubwa ambayo kila mchezaji angependa kuitumikia,” alisema Phiri.

Ujio wa Phiri ndani ya Simba ukiongeza na ufundi wa kiungo Clatous Chama ambapo wawili hao ni marafiki utaipa nguvu kubwa Simba ambayo imeanza kujenga upya kikosi chao kuelekea msimu ujao.

Phiri ambaye ana kasi na kujua kufunga akicheza kama kiungo wa pembeni mshambuliaji (winga) huku pia akiwa na uwezo wa kucheza kama mshambuliaji wa nyuma ya mshambuliaji wa mwisho, anatarajiwa kuirudishia nguvu timu hiyo baada ya kuyumba msimu huu katika mashindano ya ndani.

Simba inafanya mambo yake kimyakimya na haitaki kusema sana na usajili wao wa kwanza kwa staa wa kigeni waliyemalizana naye hadi sasa ni mshambuliaji ambaye alikuwa kipiganiwa na watani wao Yanga ni Moses Phiri.

Phiri mapema katika kipindi cha usajili mdogo uliopita alizigonganisha vichwa Simba na Yanga akikubaliana na ofa za klabu zote mbili ingawa klabu yake ya Zanaco iliweka ngumu kumwachia.

Zanaco iligoma kumuuza Phiri kufuatia kukabiliwa na mechi za kimataifa za CAF.