Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Perez alivyoinyonga Madrid

Muktasari:

Perez mmoja wa watu wenye nguvu ya kifedha barani Ulaya, maamuzi yake yanatajwa kuwa mabovu kuwahi kutokea katika historia na ndiyo yamekuwa yakiigharimu klabu hiyo inayoongoza kwa utajiri dunia kwa kuwa na thamani ya Pauni 3.4 bilioni.


REAL Madrid moja ya klabu maarufu na tajiri zaidi duniani, kwa sasa imekuwa ikikabiliana na wakati mgumu kushinda mataji huku wapinzani wao, Barcelona wakionekana kutulia na kufanya mambo kwa raha zao. Mengi yamezungumzwa kuhusiana na mwenendo mbovu wa klabu hii licha ya kuwa na wachezaji wa bei mbaya na wenye majina makubwa duniani kama Cristiano Ronaldo, Gareth Bale, Tony Kroos, Pepe, James Rodrigues, Luca Modric, Isco na wengine wengi.Kwa miaka mingi klabu hiyo imejipambanua kuwa na misuli minene katika kusajili mastaa wa dunia kwa kumwaga mkwanja mrefu, pia ni mabingwa wa kufukuza makocha. Yote haya yanaelezwa kufanyika chini ya utawala wa Rais wake Florentino Perez.

Perez mmoja wa watu wenye nguvu ya kifedha barani Ulaya, maamuzi yake yanatajwa kuwa mabovu kuwahi kutokea katika historia na ndiyo yamekuwa yakiigharimu klabu hiyo inayoongoza kwa utajiri dunia kwa kuwa na thamani ya Pauni 3.4 bilioni.

Pia ndiyo klabu yenye madeni makubwa kuliko zote duniani, ikidaiwa kiasi cha Pauni 750 milioni. Rais wake huyo anadaiwa kutumia mamilioni ya klabu kufanya usajili usiokuwa na tija kwa maana ya kusajili wachezaji wasiokuwa na mchango mkubwa huku akibadilisha makocha mara kwa mara kana kwamba, anabadili nguo.

Hata hivyo, pamoja na madudu hayo mashabiki wa Real Madrid wamekuwa wakimuona Perez kama mtu sahihi kuongoza klabu hiyo kutokana na kukata kiu yao ya kuona nyota wenye majina makubwa wanaosajiliwa kila msimu.

Hilo ni kosa kubwa sana kwa mashabiki, hebu angalia majanga mazito ambayo Perez ameyafanya katika uongozi wake na mpaka sasa yanaigharimu Real Madrid kila kukicha.


15. Vicente del Bosque

Aliichezea Real Madrid kama kiungo katika miaka ya 1970 na kushinda mataji matano ya La Liga na baadaye kuwa kocha mwenye mapenzi makubwa na klabu hiyo.

Akikinoa kikosi hicho del Bosque alibeba mataji taji la La Liga na mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini aliishia kutimuliwa wakati ambao klabu ilikuwa ikifanya vizuri. Perez ndiye alishawishi Bodi na kocha huyo mpole akatupiwa virago.

Katika kuwaonyesha kuwa walifanya uamuzi wa kipuuzi, del Bosque akakabidhiwa kikoba ya kuinoa timu ya taifa ya Hispania, ambako alimaliza nafasi ya pili katika fainali za Ulaya na kushinda Kombe la Dunia.


14. Kupigwa bei kwa Makelele

Hapa ndipo mambo yalipoanza kwenda mrama ndani ya Real Madrid. Ni hatua ya Perez kumuuza Claude Makelele kwa Chelesea mwaka 2003. 

Alikuwa kiungo mahiri mwenye kasi na anayesaka mpira na kurejesha kwa kasi kwa viungo na washambualiaji. Ndiye alikuwa injini ya kutengeneza mabao kwa safu ya ushambuliaji ya Real ikiongozwa na Raul Gonzalez.

Inaaminika kuwa majanga baina ya del Bosque na Perez yalishika kasi baada ya kuuzwa kwa Makelele, uamuzi ambao uliwashitua wachezaji na mashabiki.

Akiwa Chelsea chini ya Jose Mourinho, Makelele aliiwezesha kubeba mataji ya England mara mbili mfululizo. Kwa sasa anaogelea kwenye bwala la fedha PSG akiwa msaidizi wa Laurent Blanc.


13. Ronaldinho v Beckham

Ronaldinho akiwa kwenye kiwango bora zaidi barani Ulaya alikuwa mbioni kujiunga na Real Madrid, lakini kama kawaida Perez akafanya madudu yake.

Safari hii akavunja mpango wa kumsajili kiungo mahiri kabisa na kumgeukia mwanamitindo, David Beckham, ambaye hakuwa na cheche kama za Gaucho.

Ghafla usiyempenda kaja, Gaucho akatua Barcelona na siku chache baadaye El Classicos ikawadia na alipokanyaga uwanja wa Santiago Bernabeu akaipiga Madrid hat trick. Perez mdomo wazi huku vigogo wenzake wakimtazama kana kwamba, wanamuuliza yule ndiye Gaucho uliyesema si lolote. Uamuzi huo wa mwaka 2003 mpaka sasa umeendelea kuigharamu Real Madrid.


12. Kusajili mastaa mizigo

Usajili wa bei mbaya wa Jonathan Woodgate, Nicolas Anelka, Walter Samuel, Pedro Leon, Fabio Coentrao, Flavio Conceicao, Royston Drenthe, Antonio Cassano na Julien Faubert kwa Madrid ilikuwa ni sawa na kutumbikiza mamilioni ndani ya shimo la choo.

Ni wachezaji nyota lakini mizigo walioshindwa kuonyesha thamani licha ya kununuliwa kwa bei mbaya na kulipwa mishahara mikubwa. Perez tena akifanya mambo yake.


11. Kuwatosa Sneijder na Robben

Perez akitumia ushawishi wake aliwaruhusu nyota wawili wa Uholanzi, Wesley Sneijder na Arejn Robben kuondoka kikosini. 

Waliondoka wakiwa na viwango bora na vya juu, ambako walikuwa msaada mkubwa kwa klabu zao mpya. Sneijder aliisaidia Inter Milan kubeba mataji huku Robben akiendeleza shughuli pevu huko Bayern Munich.


10. Sera mbovu za Mourinho

Miaka minne ya Jose Mourinho ndani ya Real Madrid ilikuwa ya hovyo na kuharibu misingi ya klabu hiyo iliwekwa kwa miaka mingi. 

Alitengeneza mfumo wa kuzuia zaidi badala ya kutandaza soka safi huku akiugeza El Classicos kuwa ya vita na uhasama huku wachezaji wakicheza kwa ubabe badala ya kuonyesha kandanda safi kama ilivyozoeleka.

Licha ya kushinda La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya, Perez alishindwa kumdhibiti kocha huyo na kujikuta akiachwa madhara badala ya faida kwa klabu.


9. Nguvu ya wachezaji

Kama hufahamu ni kuwa ndani ya Real Madrid wachezaji kama Ronaldo, Segio Ramos, Karim Benzema na Pepe wana nguvu kuliko kocha.

Ukitaka kutupiwa virago ama kibarua ukakiona cha moto, basi waweke benchi wachezaji hao kisha utaona habari yake.

Hawa wana nguvu na wamekuwa wakisikilizwa na Perez na kupewa kila wanachotaka. 

Kwa kifupi wana ushawishi mkubwa kwa klabu na wakati mwingine huamua mchezaji gani asajiliwe ama kutemwa. Upuuzi kama huu huwezi kuuna ndani ya Man United chini ya Alex Ferguson ama Luis van Gaal.


8. Ujio wa Kaka

Alisajiliwa kwa dau la Pauni 74.5 milioni akitokea AC Milan kwenda Madrid mwaka 2009, baada ya kushinda mataji mbalimbali akiwa na vigogo hao wa Italia.

Miaka yake minne ndani ya Madrid haikuwa na tija kwa klabu kwani alishindwa kuonyesha kiwango chake huku akiwa majeruhi mara kwa mara.


7. Mrithi wa Iker Casillas

Tabia ya Perez kununua wachezaji wenye vipaji na majina makubwa, imezidisha madhara kwa klabu, ambapo kwa miaka mingi imeshindwa kutengeneza mrithi sahihi wa Iker Casillas.

Tangu mwaka 1999 akiwa bado kijana mdogo, Casillas alijipambanua kuwa ndiye kipa namba moja wa Real Madrid na ilikuwa hivyo hadi alipoingia kwenye mzozo na Mourinho ndipo alipolifahamu benchi likoje.

Kwa sasa lango hilo linalindwa na Keylor Navas na Real Madrid walipambana kumng’oa David De Gea kutoka Man United kama mrithi wa Casillas, lakini walikwama.


6. Kuuzwa kwa Mesut Ozil

Ilileta usumbufu mkubwa sana ndani ya Real Madrid. Kuuzwa kwa mfalme wa kutengeneza pasi za mwisho za mabao, kuficha mipira kwa muda mrefu haukuwa uamuzi sahihi hata kidogo.

Kuondoka kwake kulipunguza mabao kwa akina Ronaldo na Benzema. Kwa sasa anafanya yake akiwa The Gunners baada ya kuuzwa kwa dau la Pauni 61.7 milioni mwaka 2013.

Kwa sasa Ozil anatengeneza pasi ya bao moja kwa kila mechi anayocheza akiwa na Arsenal.


5. Kuuzwa kwa Gonzalo Higuain

Mpachika mabao wa Argentina ambaye alikuwa kwenye kiwango cha juu wakati akitupiwa virago Real Madrid, akifunga mabao 107 katika michezo 190. Alikuwa pacha mzuri wa Benzema lakini hakuwa na ushawishi kwa klabu na kuuzwa Napoli, mwaka 2013. Akiwa huko alipachika mabao 53 katika michezo 88.


4. Kuchemsha kwa De Gea

Kukosa mipango ya uhakika katika mbio za kumnasa kipa namba moja wa Man Utd, De Gea na kuondoka kwa Casillas ni pigo lingine kwa klabu.

Kwa sasa De Gea anatajwa kuwa mmoja wa makipa mahiri na bora kabisa nchini England na barani Ulaya.


3. Ushamba wa Ronaldo

Kwa nje unaweza kuwa hali ni shwari ndani ya kikosi na benchi la ufundi la Real Madrid. Ukweli ni kuwa hali ni mbaya na mambo makubwa yanaendelea. Tabia za Ronaldo kutaka kufunga mwenyewe kila mechi, imekuwa ikiwagawa nyota wa klabu hiyo.

Imefika hatua mashabiki wa klabu hiyo kumzomea Ronaldo, ambaye amevunja rekodi ya mabao klabuni hapo. 

Ronaldo amekuwa na kawaida ya kutoshangilia na wenzake pindi anapofunga goli mwingine. Hili ni tatizo kubwa, lakini Perez yuko kimya.


2. Kufukuzwa kwa Carlo Ancelotti

Muitaliano huyo aliipa Real Madrid kitu ilichokuwa ikikisaka kwa muda mrefu nalo ni taji la 10 la Ligi ya Mabingwa Ulaya. 

Hivi hilo halikuwa jambo la kumridhisha Perez? Hapana, aliamua kumtimua na kusaka kocha mwingine wa kushika mikoba yake.

Kuondoka kwake kuliibua mzozo kidogo baina ya wachezaji, lakini hali ilitulia baada ya kuingia kwa Rafa Benitez.


1.Benitez v Zidane

Kutimuliwa kwa Rafa Benitez hakukushangaza kwa sababu kwa Perez kutimua makocha imekuwa kawaida. 

Benitez akatupiwa virago katika mazingira ambayo yalishitua wengi na mikoba kukabidhiwa gwiji la zamani la klabu hiyo, Zinedine Zidane. Kwa Zinade ni kweli ana kipaji, lakini ana uzoefu wa kukinoa kikosi hicho na kutoa ushindani kwenye michuano mikubwa. Zidane ni miongoni mwa wachezaji mahiri katika kizazi hiki, lakini hana uzoefu wa kutosha wa kuwa kocha mwenye kiwango cha juu. 

Kwa maana nyingine amefukuzwa kocha mwenye kiwango, uzoefu na heshima kubwa barani Ulaya, lakini ameridhiwa na mchezaji nguli ambaye hana ujuzi. 

Huyu ndiye Perez, ambaye ukifanyika uchaguzi ndani ya Real Madrid kwa sasa atashinda kwa sababu ataahidi kuwaleta nyota kama akina Paul Pogba, Robert Lowandosk na wengine wengi.