Pawassa: Kariakoo Dabi itaamuliwa na viungo

Muktasari:

  • Akizungumza na Mwanaspoti, Pawassa amesema hiyo ni kutokana na aina ya wachezaji waliopo maeneo hayo kwa pande zote mbili na mara nyingi ndio wanaofunga na kutawala mpira.

BEKI wa zamani wa Simba, Boniface Pawassa amesema eneo la kiungo ndilo litakaloamua mechi kesho Yanga ikiikaribisha Simba kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 11:00 jioni.

Akizungumza na Mwanaspoti, Pawassa amesema hiyo ni kutokana na aina ya wachezaji waliopo maeneo hayo kwa pande zote mbili na mara nyingi ndio wanaofunga na kutawala mpira.

Amesema vikosi vyote viwili vina wachezaji wazuri eneo la kiungo na ndio waliofunga mabao mengi hadi sasa kwenye ligi akimtolea mfano Stephane Aziz Ki (14) na Clatous Chama (8).

“Eneo la kiungo ndilo litakaloamua mchezo wa kesho, ukiangalia timu zote mbili zinategemea eneo hilo kwenye michezo yao na ndio wameachangia kwa kiasi kikubwa ushindi na upachikaji wa mabao kwenye mechi zilizopita,” alisema na kuongeza;

“Kuhusu ubora wa Yanga na kupata matokeo, sijawahi kuamini kwenye hilo, naamini mbinu bora za makocha kila upande ndizo zitatoa taswira ya ushindi na ukiangalia mabenchi yote yana makocha wenye mbinu nzuri,” alisema.

Yanga mzunguko wa Kwanza iliibuka na ushindi wa mabao 5-1, jambo ambalo Pawassa anaamini mchezo wa kesho utakuwa mgumu zaidi.

Amesema Simba pia ni bora tofauti na watu wanavyoichukulia huku akiweka wazi timu hiyo inayotajwa kukosa ubora ndiyo iliyotolewa hatua ya robo fainali na ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi.