Pasi penalti: Ajibu kazaliwa upya kupiga mabao Yanga

Muktasari:

 

  • Mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajibu ametengeneza mabao 11, kati ya 14, yaliyofungwa na kikosi hicho tangu msimu wa Ligi Kuu Bara ulipoanza.

ACHANA na stori za Oktoba saba ambazo ulizisikia baada ya kufanya mambo ya ukweli pale Taifa dhidi ya Mbao FC alipopiga bao la tiktaka kwa lugha ya wenzetu wanaliita ‘ Acrobatic’ na kuipa Yanga ushindi wa mabao 2-0, juzi Jumamosi, Ibrahim Ajibu ‘Kadabra’ ameendeleza rekodi yake ya mabao msimu huu.

Ajibu juzi aliiongoza Yanga kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya timu ngeni katika Ligi Kuu Bara, Alliance FC ya Mwanza, akifunga bao moja na kutengeneza mengine mawili na kumfanya afikishe mabao 11 aliyohusika nayo.

Yanga imefunga mabao 14, lakini matatu yakifungwa na straika huyo na kutengeneza mengine nane katika mechi zake saba tu za msimu huu, hali inayoonyesha kuwa msimu huu ni kama kazaliwa upya ili kuwabeba Jangwani.

Ajibu aliyekuwa anachukuliwa kama ameanza kufulia tangu alipohama Simba msimu uliopita amekuwa akiwatetemesha mabeki na makipa wa timu pinzani, kwani amekuwa akiufanya mpira uwe mwepesi mbele yake kadri atakavyo.

Mwanaspoti inakuletea dondoo kuonyesha namna gani Ajibu amepikwa upya na Mwinyi Zahera kwa ajili ya kuizalishia mabao Yanga katika msimu huu katika mechi zao saba wakilisaka taji la 28 tangu kuasisiwa kwa Ligi Kuu mwaka 1965.

YANGA vs MTIBWA

Katika mchezo huo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-1, mabao yaliyofungwa na Heritier Makombo dakika 30 na lile la Kelvin Yondan kwa mkwaju wa penalt dakika ya 38. Ajibu alihusika kupika bao lililofungwa na Makambo, kwani Gadiel Michael alipokea mpira wa Ajibu kabla ya kumtupia Makambo aliyefanya kazi nyepesi.

Pia bao la pili, Kaseke alipokea mpira kutoka kwa Ajibu kabla ya kumwekea Mrisho ngasa aliyeanguswa ndani ya 18 na kusababishwa penalti.

YANGA vs COASTAL

Ulikuwa moja ya mchezo wenye ushindani kwa Timu zote kwa kuonyesha kandanda safi, lakini haikumzuia, Ajibu kumtengenezea, Heritier Makombo dakika 11 na kufunga bao lililodumu dakika zote 90 na Yanga kujiwekea kibindoni alama tatu.

Ajibu anaonekana kupika zaidi mabao tofauti na kufunga yeye mwenyewe ndio maana kwa haraka unaweza usimwone mara zote anapokuwa uwanjani.

YANGA vs SINGIDA UTD

Ulikuwa mchezo wa kwanza kwa Mrundi, Amisi Tambwe kurejea msimu huu, baada ya kukaa kwa muda mrefu nje, pia ndio ilikuwa siku yake ya kutoa gundu kwa kufumania nyavu kwani mara ya mwisho alifunga msimu ulipita wakati Yanga ikicheza dhidi ya Toto African Mei 16, 2017.

Katika mabao hayo ya Tambwe dakika ya 29 na 45, Ajibu alianza kutengeneza nafasi nzuri iliyomfanya Tambwe kufunga kwa kichwa kabla ya kutengeneza mazingira kwa bao la pili alipompa mpira, Kaseke ambaye alitoa pande kwa Tambwe na kukwamisha wavuni na Yanga kuibuka na ushindi wa mamboa 2-0.

YANGA vs STAND UTD

Lilikuwa bonge la ‘game’ kwani Yanga walitamani mpira uishe siku hiyo baada ya kuchezewa mpira mwingi na wapinzani wake tena dakika za mwisho Stand walikuwa watamu si mchezo, wanaliandama lango la Yanga vilivyo. Mchezo huo ulimaliza kwa Yanga kushinda kwa maboa 4-3. Siku hiyo ndio ‘Hat trick’ ya kwanza msimu huu ilitengenezwa na Alex Kitenge, lakini katika mabao manne ya Yanga, Ajibu alifunga bao moja lile la pili dakika ya 32 baada ya kuachia mkwaju wa hatari baada ya kupokea pasi ya Tshishimbi.

hata hivyo Ajibu alihusika katika upikaji wa mabao siku hiyo akianza lile la kwanza lililofungwa na Ngasa, kisha faulo iliyopigwa baada ya Makambo kufunga bao la tatu, lakini dakika ya 54 alitoa pande kwa kichwa na kumkuta, Kaseke aliyefunga bao la nne.

SIMBA vs YANGA

Mchezo wa watani ulifunika kila kona ya Mtaa, lakini ulimazika kwa suluhu iliyoibeba zaidi Yanga, haukuwa mchezo mzuri kwa Ajibu kwani hakuifanya kazi yake vyema kama ilivyotarajiwa.

Kocha, Mwinye Zahera hakutaka kujiuuliza maswali mengi alipoamua kumto, Ajibu na nafasi yake kuchukuliwa na Mateo Anthony dakika ya 55 katika mchezo huo ulioingiza watazamaji 50,168 na kufanikiwa kuvuna jumla ya Sh 404,549,000 Milioni huku Simba SC ambao walikua wenyeji wakipata Sh 194,962,105.41Milioni.

YANGA vs MBAO FC

Huu mchezo ulipigwa mwishoni mwa wiki na Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, katika mchezo huo bao la kwanza lilifungwa na Makambo dakika 16 baada ya adhabu safi iliyochongwa na Ajibu na kuwaweka kifua mbele Yanga hadi mapumziko.

Timu hizo zilirudi kumalizia dakika 45 za mwisho huku wengi wakiamini Mbao FC wanaweza kuchomoa lakini hali ilikuwa tofauti baada ya Ajibu kufanya mambo mazito dakika za nyongeza alipoipatia Yanga bao la pili.

Kwa sasa kila kona ya Mtaa wapenzi wa Soka wanalizungumzia bao hilo matata lililofungwa na Ajibu, huku wengi wakitabili kuwa linaweza kuwa bao bora msimu huu kutokana na mazingira ya bao hilo lilivyoingia nyavuni.

YANGA vs ALLIANCE

Mechi hiyo ya juzi Ajibu aliendelea kuwathibitishia mashabiki wa Yanga kuwa yupo moto kwelikweli, baada ya kutengeneza bao la kwanza kwa Makambo kwa kupiga pasi ndefu iliyomalizwa wavuni kwa kichwa katika dakika ya 17.

Wakati Alliance wakijiouliza watalirejesha vipi bao hilo, Ajibu tena alimpa pande tamu mkongwe Mrisho Ngassa aliyetumbukiza wavuni bao kwa kuubetua mpira uliopishana na kipa wa wageni hao wa Ligi Kuu.

Dakika nne kabla ya kumalizika kwa pambano hilo na huku Alliance wakionekana kucharuka kwelikweli, Deus Kaseke alipokea mpira na kupiga kwa Ajibu ambaye akiwa katikati ya mabeki wa timu pinzani alitumbukiz wavuni lao lake la tatu.

MUDA UNARUHUSU

Chini ya Kocha Mwinyi Zahera ambaye ni kocha bora wa mwezi uliopita, nyota wa Yanga wanaweza kuendelea kufanya vyema kama watakuwa makini kumsikiliza kocha huyo.

Zahera ni moja ya makocha wachacha waliofanya vyema kwenye Ligi Kuu hasa kwa Timu kongwe, Simba na Yanga kwani ndio kocha aliyeibeba Yanga ikiwa kwenye ukata mkali lakini hakujali hilo, na alifanya kazi kwa moyo wote na hilo limekuwa faida kwa kina Ajibu na wengineo.