Pamba yabanwa mbavu Nyamagana

Wednesday July 21 2021
mbavu pic
By Mgongo Kaitira
By Damian Masyenene

Timu ya Pamba SC ya Mwanza imeshindwa kuutumia vyema uwanja wake wa nyumani Nyamagana jijini hapa baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na Coastal Union ya Tanga katika mchezo wa mtoano (Playoff) uliochezwa hii leo Julai 21 uwanjani hapo.

Wageni Coastal Union ndiyo walikuwa wa kwanza kupata bao mnamo dakika ya kwanza kupitia kwa mshambuliaji wake wa kutumainiwa, Abdul Seleman (Sopu), huku wenyeji Pamba SC wakisawazisha katika dakika ya 12 kupitia kwa James Ambrose aliyeachia shuti kali lililomshinda kipa.

Pamba SC walipata bao la pili katika dakika ya 76 kupitia kwa Emmanuel Haule aliyefunga kwa mkwaju wa penalti baada ya beki wa Coastal Union kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.

Matumaini ya Pamba kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo yalizimika ghafla katika dakika za lala salama baada ya Raizin Hafidh kuisawazishia timu yake bao mnamo dakika ya 89 akimalizia mpira uliokuwa uliotemwa mlinda mlango, Deus Tilusubya.

Katika kipindi cha kwanza, Pamba SC walikosa mkwaju wa penalti uliopigwa na Elinywesya Simbu katika dakika ya tano baada ya  nahodha wa timu hiyo, Majaliwa Shaban kuangushwa katika eneo la hatari.

Wana TP Lindanda walifanya juhudi mbalimbali za kutafuta ushindi kwa kulisakama lango la Wagosi wa Kaya  ambapo katika dakika ya 29 shuti la mkwaju wa adhabu ndogo uliopigwa na Elinywesya Simbu liliokolewa na kipa wa Coastal Union, Abubakar Ibrahim na kuwa kona.

Advertisement

Mchezo huo ulianza kwa kasi, huku Pamba waliokuwa wakishangiliwa na mashabiki waliojitokeza kwa wingi uwanjani hapo wakitawala mchezo kwa kulisakama lango la wapinzani wao na kukosa nafasi nyingi za kupachika mabao, ambapo Coastal Union walikuwa wakijibu mapigo kwa mashambulizi ya kushtukiza.

Kipa wa Coastal Union, Abubakar Ibrahim alionekana nyota wa mchezo kwa kuokoa michomo mingi ya hatari iliyoelekea langoni kwake na kuendelea kuwaweka salama Wagosi wa Kaya.

Baada ya kumaliza dakika 45 bila kufanya mabadiliko ya wachezaji, kipindi cha pili timu hizo zilifanya mabadiliko, kwa upande wa Pamba SC aliingia Reward William kuchukua nafasi ya Maulid Fadhil, huku Coastal wakiwatoa Francis Mustapha na Issa Abushee na kuwaingiza Mudathir Said na Rashid Chambo.

Kufuatia matokeo hayo, sasa Pamba SC ambao wameisaka kwa muda mrefu nafasi ya kucheza Ligi Kuu, wanalazimika kusubiri hadi Julai 24, mwaka huu kujua hatma yao katika mchezo wa marudiano utakaopigwa kwenye uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Advertisement