Pamba FC na Coastal Union kipindi cha kwanza bado hakuna mbabe

Matukio katika picha kwenye mechi kati ya Pamba na Coastal Union ya Tanga unaopigwa katika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza. Mpira ni mapumziko Pamba 1-1 Coastal Union. PICHA NA MGONGO KAITIRA

Wageni Coastal Union walikuwa wa kwanza kupata bao mnamo dakika ya kwanza kupitia kwa mshambuliaji wake wa kutumainiwa, Abdul Seleman (Sopu), huku wenyeji Pamba FC wakisawazisha katika dakika ya 12 kupitia kwa James Ambrose aliyeachia shuti kali lililomshinda kipa.

Pamba FC walikosa mkwaju wa penalti uliopigwa na Elinywesya Simbu katika dakika ya tano baada ya  nahodha wa timu hiyo, Majaliwa Shaban kuangushwa katika eneo la hatari.

Wana TP Lindanda waliendelea kulisakama lango la Wagosi wa kaya wakisaka ushindi, ambapo katika dakika ya 29 shuti la mkwaju wa adhabu ndogo uliopigwa na Elinywesya Simbu liliokolewa na kipa wa Coastal Union, Abubakar Ibrahim na kuwa kona.

Mchezo huo ulianza kwa kasi, huku Pamba waliokuwa wakishangiliwa na mashabiki waliojitokeza kwa wingi uwanjani hapo wakitawala mchezo kwa kulisakama lango la wapinzani wao na kukosa nafasi nyingi za kupachika mabao, ambapo Coastal Union walikuwa wakijibu mapigo kwa mashambulizi ya kushtukiza.