Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Pacome ampindua Ahoua, malijendi wafunguka

PACOME Pict

KUNA mambo yanaendelea baada ya msimu wa Ligi Kuu Bara kumalizika, ambapo nyuma ya pazia vigogo wa timu wameanza kujifungia ili kukamilisha dili za wachezaji wapya na kupanga namna maisha yatakavyokuwa msimu ujao kwenye mashindano mbalimbali.


Ishu ya kupanga maisha ya msimu ujao inapoendelea katika kila timu itakayoshiriki ligi hiyo na zile za chini, bado kuna mnyukano mwingine unaoonekana kuanza kushika hatamu ukiwahusisha mastaa kibao wa michuano hiyo, lakini wawili tu ndio wanaotajwa kwa sasa.


Katika mnyukano huo, baada ya kuonyesha kiwango bora kwenye michezo ya mitatu ya mwisho, kiungo wa Yanga Pacome Zouazoa amepindua ufalme aliokuwa nao Jean Charles Ahoua wa Simba.

Awali kabla ya michezo ya mwisho Ahoua alikuwa akipewa nafasi kubwa ya kuzoa tuzo mbili kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu, tuzo ya mfungaji bora pamoja na Mchezaji Bora wa Ligi Kuu (MVP), lakini ghafla mambo yamebadilika.

Pacome alifanikiwa kufanya mambo makubwa kwenye michezo mitatu ya mwisho akifunga mabao mawili kwenye mechi dhidi ya Prisons, akihusika kwenye mabao mawili mchezo dhidi ya Dodoma Jiji na kuhusika kwenye mabao yote mawili mechi kati ya Yanga na Simba ambapo timu yake iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Mkapa.

Mojawapo wa vigezo vya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumpata MVP ni pamoja na namna mchezaji alivyohusika kuisaidia timu yake kupata mafanikio.

Ahoua raia wa Ivory Coast tayari ana uhakika wa kuchukua tuzo ya mfungaji bora wa ligi, akiwa amefunga mabao 16, mawili mbele ya mshindani wake Clement Mzize wa Yanga ambaye alifunga mabao 14.

Hata hivyo, sasa vita kubwa inaonekana kuwa upande wa MVP, ambapo pamoja na wachezaji wengi kutajwa, lakini jina la Pacome na Ahoua yanaonekana kuwagawa wadau wa soka nchini, lakini kasi ya Pacome mwishoni imeleta maswali mengi.

Nyota hao wote ni raia wa Ivory Coast na huko walikotoka walifanikiwa kubeba Tuzo ya MVP kabla ya kutua Tanzania wakitokea klabu za nyumbani kwao.

Pacome huu ni msimu wa pili anacheza Yanga, alitua 2023-2024, akitokea ASEC Mimosas wakati Ahoua aliyetokea Stella Abdjan, wote wamefanya vizuri kila mmoja kwa nafasi yake.

Pamoja na kuwa Ahoua ni msimu wake wa kwanza ndiye mfungaji bora na pia mmoja kati ya wachezaji waliofanya vizuri akiwa ametoa asisti tisa, hivyo amehusika kwenye mabao 25 kati ya 69 yaliyofungwa na Simba msimu huu.

Pacome amefunga mabao 12 na asisti 10 akihusika kwenye mabao 22 kati ya 83 yaliyofungwa na Yanga kwenye ligi msimu huu.

Lakini wakati wengi wakimpigia chapuo, Ahoua na Pacome katika suala la MVP, kuna wadau wanaamini kuwa staa wa Singida Black Stars, Jonathan Sowah aliyefunga mabao 13, Mzize wa Yanga aliyefunga 14, Feisal Salum wa Azam aliyetoa pasi 13 za mabao na kufunga mara nne nao wanastahili kutwaa tuzo hiyo msimu huu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wadau mbalimbali wa soka nchini, baadhi wamesema Pacome anastahili kutoa tuzo hiyo, lakini wengine wakiamini kuwa pamoja na Ahoua kukosa makombe, lakini binafsi amefanya mambo makubwa.

Kocha wa zamani wa Mtibwa Sugar na Gwambina FC, Mohamed Badru, amesema wala hana jambo la kujiuliza sana bali akiambiwa apendekeze atampa kura yake Pacome.

“Msimu huu, MVP wangu ni Pacome. Wakati Ahoua alipofunga mabao dhidi ya timu za katikati ya msimamo, Pacome alikuwa akiamua mechi kubwa dhidi ya Azam na Simba, alibeba timu katika nyakati muhimu sana,”  anasema Badru.

Badru amesema mchezaji bora ni yule anayefanya tofauti kwenye mechi ngumu na kwa mtazamo wake, Pacome ndiye aliyekuwa na ushawishi mkubwa zaidi ndani ya kikosi cha Yanga, hasa katika mechi ambazo ushindi ulikuwa mgumu kuupata.

Kwa upande wa kocha wa zamani wa Simba Queens, Matty Mseti yeye amesema Charles Jean Ahoua ni mchezaji wa daraja lingine kabisa na ndiye anastahili tuzo hiyo.

“Kwangu Ahoua ndiye MVP. Bila yeye, Simba ingekuwa na msimu mbaya sana. Ni mfungaji mzuri, anakimbia, anajituma. Japokuwa Simba imepoteza ubingwa yeye amekuwa na mchango mkubwa sana,” alisema Mseti.

Hata hivyo, beki wa zamani wa Yanga, William Mtendamema anasema Pacome anastahili kuwa MVP, huku akiamini aina ya mabao aliyofunga ni ya kiufundi zaidi tofauti na Ahoua ambaye data zake zipo juu lakini mabao mengi ni ya kutenga.

“Ni kweli data za Ahoua zipo juu, lakini asilimia kubwa ya mabao yake ni ya mipira ya kutenga, tofauti na Pacome mabao yake ni ya ufundi,” anasema.

Kocha wa zamani wa Simba Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alisema linapokuja suala la kiufundi hataki ushabiki kura yake alimpa Pacome.

“Pacome kaisaidia timu yake kuipa ubingwa, naheshimu kazi ya Ahoua lakini anapaswa kupambana kuleta mataji Msimbazi nje na data zake ambazo zipo juu,” anasema Julio ambaye ni mchezaji wa zamani wa Simba.

Kwa upande wa Sekilojo Chambua mchezaji wa zamani wa Yanga, alisema wapo wachezaji wengi waliocheza vizuri ila wawili wamemkosha zaidi kutokana na viwango vizuri ambavyo wamevionyesha.

“Pacome Zouzoua na Jean Ahoua wamecheza vizuri na wamesaidia timu zao kupata ushindi muhimu ambao uliozifanya timu kutoka sehemu moja kwenye nyingine.

“Mtu kama Pacome unaona kabisa umuhimu wake ndani ya kikosi akiwa na mpira na asipokuwa nao, amekuwa mwepesi wa kuanzisha mashambulizi na kuwasumbua wapinzani, lakini Ahoua naye kafunga sana msimu huu,” anasema.

Pamoja na kwamba bado haijatangazwa tuzo hizo zitatolewa lini, lakini chanzo cha ndani kutoka Shrikisho la Soka Tanzania kinasema kuwa utaratibu utafanyika kabla msimu mpya wa ligi haujaanza.