Pablo: Ubingwa Ligi Kuu bado tupo

Pablo: Ubingwa Ligi Kuu bado tupo

Muktasari:

  • Kocha wa Simba, Pablo Franco amesema bado timu yake ipo kwenye ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC msimu huu kwani bado ni mapema.

Mwanza. LICHA ya Yanga kubakiza pointi sita kutangaza ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC msimu huu, Kocha wa Simba, Pablo Martin amesema ni mapema sana kukata tamaa kwani kikosi chake kitapambana kuhakikisha inaweka matumaini kwenye ubingwa huo ikianza na mchezo wa kesho dhidi ya Geita Gold.

Simba itakuwa ugenni hapo kesho katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kukipiga na Geita Gold katika mchezo wa Ligi Kuu huku Mhispania huyo akiweka wazi kuwa kikosi chake kilichotua jana usiku jijini hapa hakina mabadiliko na atatumia nyota wale wale alioanza nao kwenye michezo miwili ya mwisho dhidi ya Azam FC na Pamba.

Pablo amesema anategemea mchezo huo utakuwa mzuri na mgumu kwakuwa anakutana na timu bora yenye wachezaji wazuri ikiwa kwenye kiwango kizuri kwani ilistahili kwenda nusu fainali ya kombe la Shirikisho lakini amejiandaa na vijana wake kuondoka na pointi tatu muhimu.

"Kuhusu ubingwa ni swali ambalo nimekuwa nikikutana nalo sana lakini nachoweza kusema ni kuwa tutaendelea kupambana mpaka mwisho kesho tunataka pointi tatu ili tuone mwisho wa safari inakuwaje, siyo kwamba ubingwa hauwezekani lakini tutakaza kuona nini kinawezekana, kuna mambo mengi lakini tunajitajidi kuwa professional," amesema Pablo na kuongeza;

"Ni wajibu wetu kuhakikisha tunacheza mchezo mzuri mbele ya mashabiki wetu kwasababu tulipocheza hapa na Ruvu Shooting sapoti ilikuwa kubwa sana na ya kupendeza.

"Ni mechi yangu ya pili tunakumbuka performance yetu ya mwisho hapa na kesho ni mchezo tofauti, tunakabiliana na timu nzuri yenye wachezaji wazuri, tulipocheza nao walicheza vyema na kuumudu mchezo hata walivyocheza na Yanga," amesema.

Hata hivyo kocha huyo amesema mazingira ya uwanja wa CCM Kirumba bado hayaridhishi kwa asilimia 100 kama ilivyokuwa mategemeo yake kwani bado kuna maeneo hayajaboreshwa na hakuna tofauti sana na mara ya  mwisho alivyokuja uwanjani hapo kucheza na Ruvu Shooting.