Pablo awatuliza Msimbazi, Bocco atoa neno

SIMBA  imepoteza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu Bara msimu huu kwa kipigo cha 1-0 dhidi ya Mbeya City, huku mashabiki wakionyesha kutofurahishwa na viwango vya baadhi ya nyota wao akiwamo nahodha John Bocco.

Bocco, 32, hajafunga bao lolote msimu huu na jana alikuwa na nafasi ya kufunga kwa mpira uliorudi wa penalti ya Chris Mugalu ambayo iligonga nguzo, lakini alijichanganya na mpira kudakwa na kipa Deogratius Munishi ‘Dida’.

Hata hivyo, Pablo amewapoza mashabiki wa mabingwa hao mara nne mfululizo wa Ligi Kuu akisema staa huyo na wengine watarejea katika makali yao na timu itatisha kama ambavyo imekuwa ikitawala soka la Tanzania.

Bocco ana historia ya kutisha nchini, akifunga mabao 139 ya Ligi Kuu katika misimu 14 tangu msimu wa 2008-09, na licha ya kuwa mfungaji bora wa msimu uliopita akimaliza na mabao 16, msimu huu hajafunga bao huku raundi 11 za mechi za ligi zikiwa zimekatika.

Lakini Pablo anaamini ni suala la muda tu kabla ya gari la nahodha wake halijawaka tena.

Pablo alisema kwa mchezaji hali ya kukosa nafasi za kufunga ni ya kawaida na ni suala la mpito tu hivyo anaamini atafanya vizuri.

Alisema ana imani kubwa na kila mchezaji ndani ya timu hiyo, hivyo hata Bocco anaamini mechi zijazo atafanya vizuri zaidi.

“Inatokea tu mchezaji kuna wakati inakuwa hivyo, sio kusema hajui hapana, ni namna ya mchezo unavyokuwa na ushindani wake,

“Unakuta pia mchezaji anajipanga kweli kweli kuhakikisha anafanya kile anachokitarajia akini ikitokea akakwama, inamuumiza hata yeye mwenyewe,” alisema Pablo na kuongeza:

“Bocco ni mchezaji mzuri na ndio maana ni nahodha na mimi nafahamu namna ambavyo anajisikia kutokana na msimu uliopita alivyofanya vizuri lakini kwa sasa hajafanya vile,” alisema Pablo.

Kocha huyo Mhispaniola alisisitiza kuwa, hawezi kumbeza Bocco sababu mbali na msaada wake wa miaka mingi Simba pia ni mchezaji tegemeo wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.

Bocco katika michezo aliyocheza mpaka sasa aliambulia kukosa penalti katika mchezo wa kwanza wa ufunguzi wa Ligi Kuu dhidi ya Biashara United, ambao walitoka suluhu.


BOCCO ATOA NENO

Akizungumza na Mwanaspoti, Bocco alisema anamshukuru Mungu anacheza kwenye timu kubwa iliyo na wachezaji wakubwa wenye kupambana kutwaa mataji na baada ya kubeba Kombe la Mapinduzi, wana mataji mawili ya kuyatetea.

Alisema yeye ni mchezaji mkubwa na amekuwa akisaidiana na wachezaji wenzake kuisaidia timu hiyo kufanya vizuri hivyo hajaona sababu ya kutajwa kama mchezaji ambaye ameshuka kiwango wakati bado anacheza na kufanya vizuri.

“Suala la kufunga ni bahati, muda ukifika na Mungu akipanga nifunge nitafanya hivyo, kikubwa ni kuwa miongoni mwa mastaa ambao wanacheza Simba nikipata nafasi ninaipambania timu kutetea mataji yaliyobaki, mengine muda utazungumza,” alisema.