Pablo apata wasiwasi na uwanja CCM Kirumba

Pablo apata wasiwasi na uwanja CCM Kirumba

Mwanza. LICHA ya Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kufanyiwa maboresho katika maeneo mbalimbali likiwemo la kuchezea 'Pitch', Kocha wa Simba, Pablo Franco ameonyesha wasiwasi na kueleza kuwa alitarajiwa maboresho makubwa na kuufanya uonekane tofauti na mwanzo lakini upo vilevile.

Uwanja huo ulifungwa tangu Februari 23 mwaka huu kupisha maboresho ikiwemo eneo la kuchezea, vyumba vya kubadilishia nguo, huduma ya kwanza na kupaka rangi ambapo unatarajiwa kuanza kutumika kesho kwenye mchezo wa ligi kati ya Geita Gold dhidi ya Simba huku majukwaa yakiwa hayajapakwa rangi kama ilivyokusudiwa.

Kabla ya mkutano wake na wanahabari leo jijini Mwanza kuzungumzia maandalizi ya timu yake, Pablo alifika uwanjani hapo saa 6 mchana akiambatana na Meneja wa habari, Ahmed Ally kukagua eneo la kuchezea.

Amesema hakuna tofauti kubwa sana na mara ya mwisho alipofika kucheza na Ruvu Shooting kwani alitarajia uwe bora zaidi ya hapo kwa ajili ya mchezo wa kesho na ule wa nusu fainali ya kombe la shirikisho dhidi ya Yanga Mei 28.

"Uwanja  uko kama nilivyoukuta mara ya kwanza nilitaraji utakuwa kwenye hali nzuri lakini bado kuna mazingira si ya kuridhisha sana, siyo mzuri sana mwa mchezo wa kesho hata wa nusu fainali," amesema Pablo.

Mwanaspoti limeshuhudia eneo la kuchezea (pitch) nyasi zikiwa hazijafyekwa ambapo jitihada za kuufyeka zimeanza mchana wa leo lakini hadi sasa hazijafua dafu baada ya mashine inayotumika kuharibika na ikiendelea kutengenezwa.