Otieno azikoroga Gor Mahia, KFK

Muktasari:

Otieno aliyekuwa beki wa kulia chaguo la kwanza kwenye kikosi cha kwanza Gor na timu ya taifa, alipata jeraha la goti kwenye mechi ya marudiano  ya kufuzu kushiriki dimba la CHAN 2020 dhidi ya Tanzania mwezi uliopita uwanjani Kasarani.

Nairobi. SHIRIKISHO la soka nchini FKF na klabu ya Gor Mahia zimeingia kwenye vuta ni kuvute kuhusu jeraha baya alilopata beki Philemon Otieno kipindi akiwa anaichezea Harambee Stars.
Otieno aliyekuwa beki wa kulia chaguo la kwanza kwenye kikosi cha kwanza Gor na timu ya taifa, alipata jeraha la goti kwenye mechi ya marudiano  ya kufuzu kushiriki dimba la CHAN 2020 dhidi ya Tanzania mwezi uliopita uwanjani Kasarani.
Beki huyo wa Gor alilazimika kuondolewa uwanjani baada ya dakika chache za mchezo. Tangu kipindi hicho, hajaweza kupata matibabu mwafaka huku Gor na FKF zikikodoleana macho bila ya kujali. Ripoti zinaarifu FKF ilikuwa na mpango wa kumsafirisha hadi Ufaransa ndani ya siku chache baada yake kuumia  ili akafanyiwe upasuaji lakini sasa wamekanyagia hiyo stori bila ya ufafanuzi mpaka sasa.
Sasa Gor kupitia Ofisa mku mtendaji Lordvick Aduda imeishtumu FKF kwa kumtelekeza mchezaji huyo.
“Niliwaandikia barua FKF Septemba 4 kutaka kujua mipango yao kuhusu jeraha la Philemon lakini mpaka leo hii hajanijibu.  Mchezaji huyo anahitaji matibabu ya haraka sababu anaumwa na anaishi kwa maumivu makali sasa hivi. Walipokuwa wakimhitaji kwa ajili ya majukumu ya kitaifa, walituandikia barua ila sasa hivi wamemtoka wakati wajibu wa kushughulikia matibabu yake upo mikononi mwao,” Aduda alisema.
Ofisa huyo anashindwa kuelewa ni kwa nini FKF ilimshughulikia beki Brian Mandela alipoumia akiwa kambini na timu kule Ufaransa kwenye maandalizi ya AFCON. FKF iligharimia upasuaji wa Mandela katika hospitali moja ya Ufaransa.
“Ndicho kitu kinachotushangaza, mbona yaliyofanyiwa Mandela hatuyaoni yakifanyiwa Philemon,” Aduda akahoji.
Hata hivyo, kwa upande wa FKF wanadai pamoja na Otieno aliumia akiwa analihudumia taifa, hamna sheria inayoishurutisha chombo hicho kuwajibikia majeraha ya wachezaji wa timu ya taifa.
“Hamna sheria inayosema shirikisho linapaswa kusimamia matibabu ya mchezaji anayepatwa na jeraha akiwa kwenye  majukumu ya kitaifa. Pia hatuna bima ya matibabu kwa wachezaji wa timu ya taifa. Philemon ni mchezaji mzuri, Gor wanapaswa kuona ni jinsi gani watakavyoweza kumsadia Shirikisho sasa hivi haina hela, kama zingelikuwepo basi tungelimsaidia” alisema afisa mawasiliano wa FKF, Barry Otieno.
Upasauji huo kurekebisha ufuniko wa goti lake Otieno unahitaji kiasi kisichopungua Sh500,000.