Olunga amuwashia moto Iniesta

UNAMKUMBUKA yule fowadi wa timu ya taifa la Kenya ‘Harambee Stars’, Michael Olunga ambaye alizamisha jahazi la Taifa Stars kwenye mchezo wa makundi wa fainali za Mataifa ya Afrika kule Misri? Unaambiwa jamaa ameuwasha moto huko mbele ya Andres Iniesta.

Olunga ambaye anacheza soka la kulipwa Japan akiwa na Kashiwa Reysol alikutana na Iniesta kwenye mchezo wa Ligi Kuu nchini humo na kuisambaratisha Vissel Kobe anayoichezea kiungo huyo fundi wa zamani wa FC Barcelona na timu ya taifa la Hispania.

Akiwa na jezi nambari 14 mgongoni, Olunga aliitanguliza klabu yake ya Kashiwa Reysol kwa kufunga bao la kwanza kwenye mchezo huo dakika ya 20 akimalizia pasi ya Cristiano.

Dakika 19 baadaye, chama la Olunga likapata bao la pili kupitia kwa Ataru Esaka kabla ya mfungaji wa bao la kwanza kurudi tena kambani kwa kufunga bao la tatu na la pili kwake kwenye mchezo huo.

Alikuwa ni yule yule Olunga ambaye aliifanya Kashiwa Reysol kwenda mapumziko wakiwa vifua mbele huku Vissel Kobe ya Iniesta ambaye alicheza dakika zote za mchezo wakiwa vichwa chini.

Kabla ya hata kutulia mwanzoni mwa kipindi cha pili, Vissel Kobe walijikuta wakiruhusu bao la nne, chama hilo la Iniesta lilijitutumua na kufunga mabao matatu kabla ya mchezo huo kumalizika.

Mbali na Junya Tanaka aliyefunga mabao mawili ya Vissel Kobe, Iniesta naye aliifungia bao klabu hiyo kwa mkwaju wa penalti.