Nyota ya Mbongo yang’ara Ligi China
Muktasari:
- Francis ameibuka kuwa mchezaji mwenye asili ya Tanzania kucheza Ligi Kuu ya China ‘Supa Ligi’, beki huyo ambaye muda mwingine huitwa Aidi Fulangxisi ni mtoto wa Mtanzania ambaye anaichezea Shanghai Shenhua.
WABONGO wanaendelea kupenya mwanangu na kutengeneza rekodi tamu, kipindi kile cha Kombe la Dunia kule Russia alikuwa Yussuf Poulsen lakini safari ni Eddy Francis.
Francis ameibuka kuwa mchezaji mwenye asili ya Tanzania kucheza Ligi Kuu ya China ‘Supa Ligi’, beki huyo ambaye muda mwingine huitwa Aidi Fulangxisi ni mtoto wa Mtanzania ambaye anaichezea Shanghai Shenhua.
Shanghai Shenhua ni ile klabu ambayo mwaka 2012 ilionyesha uthubutu na kuwanasa mastaa mbalimbali waliotikisa kwenye soka wakiwemo, Didier Drogba na Nicolas Anelka.
Mtanzania huyo ameanza kuichezea klabu hiyo mwaka huu na tangu amejiunga nayo amekuwa mchezaji muhimu kwenye safu ya ulinzi na mpaka sasa amecheza jumla ya michezo 11 ya Supa Ligi.
Francis ambaye anacheza kama beki wa kati na muda mwingine wa kushoto kutokana na kutumia kwake zaidi mguu wa kushoto, alizaliwa Shanghai, China. Mama yake ni Mchina na baba yake ni Mtanzania.
Alianza kucheza soka kwa kujiunga na Akademi iitwayo Genbao alipokuwa na umri wa miaka 10, mwishoni mwa mwaka 2005 alijiunga na Shanghai East Asia pamoja na wachezaji wenzake ambao alikuwa nao kwenye kituo hicho cha soka.
Francis alianza kupata nafasi ya kucheza kwenye timu hiyo kuanzia mwaka 2010 baada ya kurejea kwa mara ya pili akitokea Suzhou Trips iliyokuwa Ligi Daraja la Pili China na baadaye akatimkia Ureno ambako aliichezea Boavista kabla ya kutua Shanghai Shenhua.
Beki huyo mwenye asili ya Tanzania anacheza timu moja kwa sasa na mshambuliaji wa Kisenegal, Demba Ba ambaye aliwahi kuzichezea Chelsea na Newcastle United za England.
Poulsen ambaye alikuwa gumzo wakati akiitumikia Denmark katika fainali za Kombe la Dunia kule Russia alizaliwa na mama Mdenishi na baba Mtanzania Mdigo wa Tanga aliyekuwa akifanya shughuli zake za ubaharia, Kwa sasa baba huyo ni marehemu.