Nyota hawa wasipojipanga wanalo

KOCHA humpa mchezaji nafasi ya kucheza kutokana na jitihada anazoonyesha, juhudi binafsi pamoja na kumudu ushindani wa namba uliopo kwenye nafasi anayoicheza.

Wapo wachezaji walifanya vyema msimu uliopita na kugonga vichwa vya habari wakati wa usajili na kufanikiwa kupata timu mpya ambazo wanazitumikia kwa sasa.

Bahati ilioje kwao kupata timu mpya - tena zenye ubora mkubwa ambazo ni ndoto ya kila mchezaji kuzichezea. Bahati mbaya kwao ni kuhakikisha wanakuwa kwenye ubora uliozoweleka.

Timu walizotua wamekutana na ushindani mkubwa wa namba na kuwafanya waanzie benchi, ilhali wengine hata hilo benchi wanalisikia kwa mbali. Ndio, wanatakiwa kukazana na sio kubweteka maana watarudi walikotoka. Hawa hapa ni baadhi yao.

Waziri Junior - Yanga

Alikuwa ingizo la tatu ndani Yanga akitokea Mbao FC iliyoshuka daraja. Hii ni kutokana na uwezo mkubwa aliouonyesha akiwa na Mbao hasa katika safu ya kucheka na nyavu.

Yanga ilikuwa ikihaha kwenye safu hiyo na kutua kwake ilikuwa kama mmoja wa wachezaji ambao watamaliza tatizo hilo, lakini kutua kwa kina Michael Sarpong na Sogne Yacouba kunazidi kuzima nafasi yake.

Junior aliyemaliza msimu uliopita akiwa na mabao 13 ambayo yalimfanya awe nafasi ya pili katika orodha ya wafungaji wa ligi akilingana na Peter Mapunda.

Awesu Awesu- Azam FC

Machi 19, 2017 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, Madini FC ilikutana na Simba kwenye mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho (sasa Kombe la Azam), ambapo Awesu alionyesha kiwango kikubwa ambacho bila shaka ilikuwa tiketi yake ya kuondoka kwenye timu hiyo ya Ligi Daraja la Pili (SDL).

Kwa sasa amejifunga miaka miwili kuitumikia Azam FC akitokea Kagera Sugar aliyoiwezesha kumaliza katika nafasi ya nane ikivuna alama 52 kwenye michezo 38 waliyocheza msimu uliopita.

Alimaliza msimu akiwa na mabao matano, na alikuwa mmoja wa viungo bora kwenye ligi, kiwango ambacho kilikuwa mwendelezo tangu akiwa Singida United.

Tangu ametua Azam amekutana na mafundi zaidi yake na kumfanya kukosa namba ya uhakika ndani ya kikosi cha Kocha Aristica Cioaba na kujikuta akiwa anatokea benchi.

Charles Ilanfya - Simba

Historia yake inataka kufanana na ile ya kina Adam Salamba na Marcel Kaheza ambao waliwika kwenye timu nje ya Simba, lakini walipotua Msimbazi wakakutana na wanaume wa shoka ambao hata kocha kuwaweka benchi ilikuwa vigumu.

Ilanfya ametua Simba iliyojaa washambuliaji wa kutosha - kuna John Bocco, Chris Mugalu na Meddie Kagere ambao kwa mfumo anaoupenda Kocha Sven Vandenbroeck kumtumia mshambuliaji mmoja, hao wote wakae benchi ndipo Ilanfya acheze.

Ilanfya alikuwa mfalme akiwa Mwadui FC msimu wa mwaka 2018/19 kisha msimu uliopita akiwa KMC, lakini hapo alipofika anatakiwa kupambana zaidi ili kumshawishi kocha.

Peter Mapunda - Dodoma Jiji

Baada ya kumaliza shule ya sekondari mwaka 2010 pale Songea Boys, alifanikiwa kujiunga na kikosi cha vijana cha Majimaji FC lakini Kocha Kally Ongala ambaye alitambua kipaji chake alimpa nafasi ya kucheza kikosi cha wakubwa.

Alidumu hapo misimu miwili na kutimkia Mbeya City iliyokuwa imepanda Ligi Kuu na hapo alidumu kwa misimu miwili kabla ya kurudi tena Majimaji, kisha kurejea kwa mara ya pili Mbeya City hadi msimu uliopita.

Alimaliza msimu uliopita akiwa na mabao 13 akishika nafasi ya pili kwenye orodha ya wafungaji wa ligi nyuma ya Meddie Kagere aliyenyakua kiatu cha ufungaji bora kwa mara ya pili akifunga mabao 22.

Mapunda aliingia kwenye soko zuri la usajili na kutua Dodoma Jiji iliyopanda Ligi Kuu, lakini hadi sasa timu hiyo imecheza michezo mitano, ila nafasi yake imekuwa finyu chini ya Kocha Mbwana Makata, aliyemuanzisha mechi mbili huku tatu akitokea benchi.

Ibrahim Ame- Simba

Klabu ya Simba SC ilimtambulisha beki huyu wa kati kutoka Visiwani Zanzibar ambaye msimu uliopita alikuwa akikichezea kikosi cha Coastal Union ya Tanga akitikisa dimba la kati sambamba na Bakari Mwanyeto aliyetua Yanga.

Ame anatakiwa kufanya kazi ya ziada ya kuwaweka benchi Joash Onyango ‘Berlin Wall’, Pascal Wawa, Erast Nyoni na Kennedy Juma jambo linalomfanya kuwa na safari ndefu kupata namba ya uhakika.

David Kameta- Simba

Ukipenda utamwita ‘Duchu’. Ni beki namba mbili huko Simba akiwania namba na Shomary Kapombe ambaye kila kocha anayetua Msimbazi amekuwa akimwamini kutokana na kazi kubwa anayofanya.

Msimu uliopita nafasi hiyo ilikuwa kama sio Kapombe basi aliishika Haruna Shamte aliyesajiliwa kutoka Lipuli FC kama ilivyo kwa Duchu, lakini ushindani ukamshinda na sasa ana uhakika wa namba huko Namungo FC, ila sasa ni zamu ya Duchu kunyoa au kusuka.