Nyota Coastal afichua siri yake na makocha

Muktasari:
- Nyota huyo ambaye anaitumikia Coastal Union kwa msimu wa tatu sasa, anakumbukwa kwa rekodi nzuri aliyoiweka akiwa KVZ ya Zanzibar alipoibuka mfungaji bora wa ligi kuu visiwani humo kwa mabao 15 msimu wa 2021-22.
STRAIKA wa Coastal Union, Maabad Maulid amekiri kuanza kwa ugumu Ligi Kuu Bara msimu huu, huku akifichua siri ya kuaminiwa na makocha wanaotua kikosini humo na kutoa matumaini kwa mashabiki.
Nyota huyo ambaye anaitumikia Coastal Union kwa msimu wa tatu sasa, anakumbukwa kwa rekodi nzuri aliyoiweka akiwa KVZ ya Zanzibar alipoibuka mfungaji bora wa ligi kuu visiwani humo kwa mabao 15 msimu wa 2021-22.
Katika msimu uliopita, staa huyo alikuwa na mwenendo mzuri kwa kufunga mabao tisa huku akijihakikishia namba kikosini na kuiwezesha Coastal Union kumaliza katika nafasi ya nne.
Maabad ameonekana kuaminiwa na makocha waliopita Coastal Union akiwemo Juma Mgunda, Mwinyi Zahera, David Ouma na sasa Juma Mwambusi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Maabad alikiri msimu huu haujawa mzuri kwake lakini kiu yao ni kuona timu ikifanya vizuri.
Alisema mabao matatu aliyonayo hadi sasa si kiwango chake kama ambavyo amezoea kwenye soka la ushindani, akieleza kuwa kwa sasa anaenda kujitafuta upya kuhakikisha kila mechi anayopata namba anatupia.
"Kasi yangu haijapotea kihivyo labda kwenye ufungaji mabao, lakini bado ni mapema, lolote linaweza kutokea, kimsingi ni kupambana katika mechi zilizobaki nipate mabao kadri nitakavyopata nafasi.
"Mabeki wamekuwa makini na katili katika kuepuka kuruhusu mashambulizi, lakini nashukuru makocha wote wanaokuja kikosini wameniamini hivyo lazima nionyeshe kitu cha ziada," alisema nyota huyo.
Kuhusu siri ya uhakika wa namba, straika huyo alisema kujituma na nidhamu ya mchezo ndani na nje ya uwanja ndio kilichompa nafasi zaidi kuweza kupenya dhidi ya wenzake.