Niyonzima hatihati kuwavaa Biashara

WAKATI kikosi cha Yanga kikiendelea na mazoezi kujiandaa na mechi dhidi ya Biashara United, kiungo mshambuliaji wa timu hiyo Haruna Niyonzima ameshindwa kuungana na wenzake kutokana na afya yake kutokuwa nzuri.

Niyonzima katika mchezo uliopita dhidi ya KMC alitokea benchi kuchukua nafasi ya Tuisila Kisinda, ambapo tangu mazoezi ya juzi Jumanne nyota huyo raia wa Rwanda hajafanya na wenzake.

Yanga hadi sasa iko jijini Mwanza, ambapo mazoezi ya kwanza baada ya mechi na KMC waliyoshinda mabao 2-1 ilifanyia dimba la CCM Kirumba, juzi Jumanne wakajifua viwanja vya Chuo cha Ualimu Butimba na jana Jumatano asubuhi walikuwa dimba la D.I.T huko Ilemela.

Akizungumza na Mwanaspoti, meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh alithibitisha kiungo huyo kutofanya mazoezi kwa siku mbili mfululizo akieleza kuwa anasumbuliwa na malaria.

Alisema kwa sasa anaendelea na dozi, huku akisisitiza kuwa ishu ya kukosekana katika mechi yao na Biashara United itakayopigwa Jumamosi haijafahamika na itategemea na hali yake siku ya mechi.

Meneja huyo aliongeza kuwa mbali na nyota huyo, wachezaji wengine wanaendelea vyema kujiweka fiti chini ya kocha mkuu, Cedrick Kaze na matarajio yao ni kufanya vizuri.

Alisema kwa sasa akili na nguvu zote zinafikiria zaidi mchezo ujao dhidi ya Biashara United na kuwa mkakati wao ni kuona kila mechi wanapata pointi tatu na kujiweka katika nafasi nzuri ya kuwania ubingwa.

“Wengine wanaendelea vizuri na kesho Alhamisi (leo) timu itafanya amzoezi Uwanja wa Chuo cha Butimba kabla ya Ijumaa kuondoka kuelekea mjini Musoma tayari kuwakabili wapinzani,” alisema meneja huyo.