Niyonzima apata ajali Rwanda

Niyonzima apata ajali Rwanda

Muktasari:

  • Mchezaji wa Yanga na nahodha wa Rwanda, Haruna Niyonzima amenusurika kwenye ajali ya gari eneo Nyamata jijini Kigali.

MWANASPOTI limejiridhisha kwamba kiungo fundi wa Yanga na nahodha wa Rwanda, Haruna Niyonzima amenusurika kwenye ajali ya gari alilokuwa akiendesha  wakiwa akirejea kutoka Wilayani  Bugesera kuja jijini Kigali.

Kiungo wa Yanga na nahodha wa timu ya Taifa Rwanda, Haruna Niyonzima.

Awali kabla ya Mwanaspoti kuzungumza nae Niyonzima mwenyewe moja kwa moja, chanzo kilisema ajali hiyo ilitokea  eneo Nyamata.

Chanzo cha Mwanaspoti kilieleza kuwa ajali hiyo ilitokea jana wakati gari aina ya Fuso ilivyokuwa ikijaribu kuipita baiskeli ambayo ilikuwa mbele katika harakati hizo ndipo ikaigonga gari ya   Niyonzima aliyekuwa na washikaji wengine watatu.

Kiungo wa Yanga na nahodha wa timu ya Taifa Rwanda, Haruna Niyonzima.

Akizungumza na Mwanaspoti muda mfupi uliopita Niyonzima ambaye ni mchezaji wa zamani wa Simba, alisema wametoka salama kwenye ajali hiyo na hakuna mtu aliyepata majeraha miongoni mwao.

"Niligongwa lakini jambo jema ni kwamba nipo salama,kilichoumia labda ni gari lakini hakuna hata mmoja ambaye aliumia kwenye ajali hiyo,niko salama,"aliongeza staa huyo wa zamani wa APR ya hapa Rwanda

"Nilikuwa natoka kwenye mizunguko yangu ya kawaida, sasa wakati narejea nyumbani ndio yakatokea hayo,"alisema kiungo huyo aliyekuja hapa Rwanda kuichezea timu ya Taifa dhidi ya Cape Verde kuwania kufuzu Afcon lakini mechi zote mbili nyumbani na ugenini wakaambulia suluhu.

Kuhusu lini atarejea Tanzania kuendelea na majukumu yake Yanga, Niyonzima alisema anatarajia kesho Ijumaa kurejea baada ya mambo yake ya kifamilia kukaa sawa. "Kuna mambo ambayo nilikuwa naweka sawa ya kifamilia ambayo yamekaa sawa. Narudi kazini Yanga sasa." Kwa taarifa zaidi endelea kufuatilia mitandao yetu ya kijamii leo Alhamisi pamoja na Gazeti la Mwanaspoti Kesho Ijumaa kwa Sh500 tu.

_____________________________________________________________

MWANDISHI WETU,KIGALI