Ninja amtaja Bocco akijifunga

JAPOKUWA Nahodha wa Simba, John Bocco bado hajafungua akaunti yake ya mabao msimu huu kwenye Ligi Kuu Bara, imeelezwa ana mashambulizi ya kushitukiza ambayo ni hatari zaidi.

Beki aliyepelekwa na Yanga kwa mkopo Dodoma Jiji, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ alisema chanzo cha kujifunga alikuwa anawahi kuiondoa mipango ya Bocco aliyekuwa anauwahi mpira ili afunge kwa kichwa.

Alieleza namna Bocco ambavyo ni hatari zaidi anapokuwa ndani ya 18, akisisitiza asichukuliwe poa na kwamba yeye ni shuhuda wa kujua usumbufu wa staa huyo, ambaye kwa sasa hana bao katika mechi ambazo timu yake imecheza.

“Ni rahisi kumuona Bocco kaisha, ila niwaambie mabeki wenzangu wasimpuuze maana ipo siku atawaumbua, ana hesabu nyingi kila eneo analokaa,”

“Sababu ya kujifunga ilitokana na Bocco kuwa eneo la kuupiga mpira kwa kichwa, lengo langu nilikuwa nakwenda kuuwahi ili kuutoa nje, maana hata ningesimama tu bado wangeona sijaruka, hizo ni changamoto za kazi.”

Ukiachana na Bocco, alisema licha ya kwamba ni mapema lakini Moses Phiri ni straika anayejua kukaa kwenye nafasi na ana mikimbio sahihi.