Mida ya Simon Msuva kupiga mkwanja

Muktasari:
- Nyota huyo wa zamani wa Wydad AC anatarajiwa kuondoka klabuni hapo mwishoni mwa msimu baada ya mkataba wake kumalizika na mtu wa karibu na mshambuliaji huyo wa Taifa Stars amefichua kuna ofa nono mezani.
MSHAMBULIAJI Simon Msuva anayekipiga Al Talaba ya Ligi Kuu ya Iraq, Iraq Stars League, anamaliza mkataba wake na klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu na inaelezwa anatakiwa na klabu za Misri na Saudi Arabia kutokana na kuvutiwa na kiwango chake.
Nyota huyo wa zamani wa Wydad AC anatarajiwa kuondoka klabuni hapo mwishoni mwa msimu baada ya mkataba wake kumalizika na mtu wa karibu na mshambuliaji huyo wa Taifa Stars amefichua kuna ofa nono mezani.
Tangu amejiunga na Talaba msimu huu akitokea Al Najma Ligi daraja la kwanza Saudia, amekuwa na kiwango bora na katika mechi 11 amefunga mabao 12, sawa na wastani wa bao moja kila mechi.
Msuva pia yuko katika mbio za kuwania kiatu cha ufungaji na kwa mabao hayo zikiwa zimesalia mechi sita kuna uwezekano akaongeza mengine na kumfikia na kumpita anayeongoza, Ali Muhanad wa Al Shorta mwenye 23.