Ni Ruvu Shooting vs Kilombero Soccer Net fainali U20 Moro

Ruvu Shooting U20 na Kilombero Soccer Net zitakutana katika fainali ya michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 20 wilaya ya Morogoro 2022 kusaka bingwa wa michuano hiyo baada ya timu hizo kupata ushindi kwa mbinde katika michezo ya nusu fainali uwanja wa Sabasaba mkoani hapa.

Makocha wa timu hizo wanaingia katika mchezo huo wa fainali kwa kila mmoja akihitaji ushindi ili kuibuka ubingwa kutokana na timu hizo kuwa na wachezaji wenye vipaji kibao vya soka na aina ya kukuza na kuendeleza vijana hao katika mchezo huo ambapo fainali hiyo itapigwa tarehe 15 mwezi huu.

Akizungumza na Mwanaspoti ,leo Juni 12 mjini hapa, Kocha mkuu wa Kilombero Soccer Net, Catis Tully amesema mchezo wao dhidi ya Motasoa Academy katika hatua ya nusu fainali waliwadharau wapinzani wao kutokana na kufuatia michezo waliokutana nao wapinzani wao waliangushia vipigo vikali lakini mchezo huo wakalazimika kutoa kwa njia ya matuta 10-9 baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika 90.

Tully amesema wanajipanga kucheza fainali dhidi ya timu ngumu ya Ruvu Shooting iliyosheheni vijana wenye vipaji vya soka lakini na wao wana timu nzuri yenye vijana kama wao wanaocheza soka la kufundishwa.

“Tumewaona Ruvu Shooting katika michezo yao wako pamoja kwa muda mrefu, wanalala sehemu pamoja, wanachagua wachezaji wazuri wenye vipaji wanakwenda kwao ni timu iliyokamilika kwa kila kitu hivyo tunajipanga kimbinu, kisaikolojia na yoyote anaweza kupata matokeo kwa sababu nasi tuna vijana wazuri zaidi yao na dakika 90 ndio itaamua.”amesema Tully.
Tully amesema fainali itakuwa na mpira wa nguvu. spidi kubwa na kila mmoja atachukua tahadhari katika kuwazuia, kuwapita walinzi ili kupata matokeo.

Ruvu Shooting ilijihakikishia kutinga fainali kwa washambulia wao, John Chinguku kufunga bao dakika ya 16 na Haruna Fadhili akihitimisha kufunga bao la pili na ushindi dakika ya 749 huku Burkina Fc wakipata pekee kupitia kwa, Beno Matola aliyefunga dakika 73.

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Ruvu Shooting, Frank Msese amesema wanatumia michezo hiyo kama sehemu ya kujiandaa na mashindano ya Uhai Cup itayofanyika mwanzo wa Julai Jijini Dar es Salaam.

“Vijana wetu wameonyesha uwezo mkubwa katika vipaji vya soka michezo hii ya vijana U20 na tunatumia kama sehemu ya maandalizi ya michuano ya Uhai Cup 2022 inayoshirikisha timu za vijana kwa timu zilizopo ligi kuu Tanzania bara na kundi letu kuna Mtibwa Sugar, Dodoma Jiji na Mbeya Kwanza hivyo endapo tutatwaa kombe hili na tutaingia kwenye michuano hiyo kwa kujiamini na morali ya juu.”amesem Msese.

Katibu wa chama cha soka wilaya ya Morogoro (MDFA), Geofrey Mwatesa amesema ya mchezo wa fainali yamekamilika pamoja na zawadi za washindi.