Ngumi Jiwe yaiondoa Pwani Youth Sports Foundation kutinga nusu fainali michuano ya vijana U20 Morogoro

Kikosi cha timu ya vijana ya Pwani Youth Sports Foundation kilichoshindwa kufuzu kuingia hatua ya nusu fainali ya michuano ya vijana U20 wilaya ya Morogoro 2022 baada ya kukubali kuchapwa bao 3-1 na Burkina Fc katika hatua ya robo fainali maarufu ‘Ngumi Jiwe’ katika uwanja wa Sabasaba mkoani hapa. Picha na Juma Mtanda.

Muktasari:

  • Michuano hiyo ilianza kutimua vumbi April 25 na Juni 15 mwaka huu itafika tamati ikishirikisha jumla ya timu 21 na kati ya timu hizo, tatu zimealikwa ikiwa ni pamoja na Ruvu Shooting U20, Pwani Youth Sports Foundatin na Kilombero Soccer Net na timu wenyeji 18.

Pwani Youth Sports Foundation imeaga kinyonge na kushindwa kutinga kufuzu nusu fainali ya michuano ya vijana U20 wilaya ya Morogoro 2022 baada ya kukubali kuchapwa bao 3-1 na Burkina Fc katika hatua ya robo fainali maarufu ‘Ngumi Jiwe’ katika uwanja wa Sabasaba mkoani hapa.

Burkina Fc iliyowahi kucheza ligi daraja la kwanza na kushuka daraja miaka mitano iliyopita ilianza kupata bao la kwanza kupitia kwa, Majid Abdul akifunga bao dakika 32 huku, Beno Matola akiongeza bao la pili dakika ya 65 na Shaibu Salum akihitimisha kwa kukwamisha bao la tatu na ushindi dakika ya 87 na Pwani walipata bao la kufutia machozi dakika ya 56 na, Nelson Nicras.

Kufuatia ushindi huo inaungana na Kilombero Soccer Net, Ruvu Shooting U20 kutinga nusu faili baada ya kushinda michezo yao ya robo fainali.

Akizungumza na Mwanaspoti mjini hapa, Katibu wa chama cha mpira wa miguu wilaya ya Morogoro (MDFA), Geofrey Mwatesa amesema mpaka sasa tayari zimefuzu kwa kuingia hatua ya nusu fainali baada ya kushinda michezo yao ya robo fainali ya michuano hiyo ya U20 wilaya ya Morogoro 2022.

Mwatesa ametaja timu zilizofuzu kutinga hatua ya nusu fainali kuwa ni Kilombero Soccer Net iliyoiondoa Chamwino Youth kwa bao 2-1 huku Ruvu Shooting U20 ikiitambia Fountain Gate Academy kwa bao 1-0 na Burkina Fc ikitamba mbele ya Pwani Youth Sports Foundation kwa kuichapa bao 3-1.

“Michuano hii ina lengo la kuchagua wachezaji wa kuunda timu ya vijana ya U20 wilaya ya Morogoro kwa ajili ya timu yetu kukaa stendibai kwa michuano ya TFF.”alisema Mwatesa.