Ngorongoro watengea wanariadha, milioni 7

Waandaaji wa mbio za Ngorongoro wametenga Sh7.4 milioni kwa ajili ya kuwazawadia wanariadha watakaoshinda katika mbio zao.

Mbio hizo zinatarajia kufanyika Septemba 25 mwaka huu katika barabara inayotoka gate la kuingilia hifadhi ya Ngorongoro hadi uwanja wa mazingira Bora ulioko Karatu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 22, Mkurugenzi wa Taasisi ya Michezo ya Meta,  Meta Petro amesema kuwa wametenga Sh7.4 milioni kwa ajili ya kuwazawadia washindi wa mbio hizo.

Alisema kuwa kwa upande wa kilomita 21, mshindi wa kwanza atazawadiwa Sh1 milioni,  wa pili atapewa Sh500,000 na wa tatu atajipatia Sh250,000 na wanaofuata watazawadiwa Sh150,000, 100,000 huku wa sita hadi wa kumi watapewa Sh50,000 kila mmoja.

"Kwa upande wa kilomita 10, washindi watazawadiwa Sh300, 000 , 200,000 , 100, 000 , 60,000, na 50,000 huku washindi wa sita hadi wa 10 wakipewa Sh40,000" alisema Meta.

Meta alisema kuwa kipengele cha kilomita tano washindi wa kwanza watapewa Sh200,000 na wapili akipewa Sh100,000 na wa tatu Sh50,000 huku wa nne hadi wa 10 wakizawadiwa Sh30,000.

"Tunatarajia zaidi ya wanariadha 2000 kutoka Tanzania, Kenya na Uganda ambapo mbali na fedha kwa washindi, lakini washiriki wote watapewa fulana na medali,"


Naye Katibu wa Chama cha Riadha mkoa wa Arusha, Rogath Steven alisema kuwa wameungana na waandaaji wa mbio hizo ili kufanikisha kuvuna wanariadha wenye vipaji.

"Mashindano haya yamekuwa na faida kubwa kwetu, kwani yanatukutanisha na vipaji vipya kila Mara za wanariadha ambao tumekuwa tukiwatumia katika kukuza na kuwaonyesha fursa ya kuwaendeleza lakini pia kupata wanariadha wapya watakaotuwakilisha kitaifa na kimataifa"

Rogath alitumia nafasi hiyo, kuwaalika wanariadha na wakimbiaji kushiriki mashindano hayo, pia vijana chipukizi wanaotaka kuonyesha vipaji vyao kutoka maeneo mbali mbali nchini.