Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ngoma nzito Kirumba, Azam yaitafuta rekodi ya Yanga

Muktasari:

  • Mechi hiyo ya kukata na shoka inazikutanisha timu hizo leo Jumapili kabla ya kukutana tena katika pambano la raundi ya pili la Ligi Kuu Bara litakalopigwa Juni 24, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar linaloashiria mbio za ubingwa.

JIJI la Mwanza litashuhudia nusu fainali ya pili ya Kombe la CRDB itakayozikutanisha matajiri wa Dar es Salaam, Azam FC dhidi ya Yanga, katika mechi kali na ya kusisimua itakayopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba kuanzia saa 9:30 za jioni.

Mechi hiyo ya kukata na shoka inazikutanisha timu hizo leo Jumapili kabla ya kukutana tena katika pambano la raundi ya pili la Ligi Kuu Bara litakalopigwa Juni 24, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar linaloashiria mbio za ubingwa.

Timu hizo zinakutana leo ikiwa ni tangu mara ya mwisho zilipokutana Aprili 25, 2026, katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Muungano iliyopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar na Yanga kuibuka kidedea na ushindi wa mabao 2-1.

Bao la Azam lilifungwa na Feisal Salum ‘Fei Toto’ huku ya Yanga yakifungwa na Prince Dube na Maxi Nzengeli na kuipeleka fainali timu hiyo na kushuhudiwa ikishindwa kutamba baada ya kuchapwa 1-0, dhidi ya watani zao Simba, Aprili 29, 2026.

Baada ya siku 57, tangu mara ya mwisho Azam FC na Yanga zilipokutana visiwani Zanzibar, hatimaye miamba hiyo miwili leo inakutana tena katika mechi kali ya ushindani kutokana na aina ya wachezaji bora na wazoefu iliokuwa nao.

Yanga ambao ni mabingwa wa Kombe la CRDB kwa misimu minne mfululizo, inaingia katika mechi hiyo ikiwa na rekodi nzuri tofauti na wapinzani wao Azam, kwani kikosi hicho hakijapoteza pambano lolote la mashindano hayo tangu Julai 25, 2021.

Yanga ilichapwa na Simba bao 1-0 lililofungwa na Taddeo Lwanga dakika ya 80, katika mechi ya fainali ya michuano hiyo kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma na haijapoteza hadi leo unaposoma habari hii, ikiwa inatimiza siku 1792, ikiwa ni miaka mitano, miezi 10 na siku 27, rekodi ambayo Azam FC ina kazi ya kuivunja

Yanga imecheza jumla ya mechi 28 za Kombe la CRDB na safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho imefunga mabao 84, huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 10.

Azam pia imekutana na Yanga mara mbili katika Kombe la CRDB na kuchapwa mechi zote tena za fainali, ikianza na ya bao 1-0, lililofungwa na Mzambia Kennedy Musonda kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga Juni 12, 2023.

Timu hizo zikakutana tena hatua ya fainali ya Kombe la CRDB msimu wa 2023-2024 na Yanga ilishinda kwa penalti 6-5, baada ya suluhu (0-0) ya dakika 120, katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Juni 2, 2024.

Kwa maana hiyo, Azam FC inakabiliwa na rekodi ngumu ya kuivunja leo kwa Yanga na kuandika historia mpya, kabla ya timu hizo hazijakutana tena katika mechi ya raundi ya pili ya Ligi Kuu Bara itakayopigwa visiwani, Zanzibar, Juni 24, 2026.


SAFARI ILIVYOKUWA

Katika michuano ya CRDB msimu huu wa 2025-2026, timu hizi zote zilianzia hatua ya 64 bora na Yanga ilianza kampeni za kutetea taji hilo kwa kuichapa Cosmopolitan mabao 2-0, huku Azam FC ikiifunga Endument FC kutoka Kilimanjaro bao 1-0.

Raundi ya 32, Yanga ikakutana na kikosi cha maafande wa Polisi Tanzania na kukitembezea kichapo kikali cha mabao 7-1, huku Azam FC ikiifunga Mbeya Kwanza bao 1-0 na timu hizo zote zilizopoteza zinashiriki Ligi ya Championship.

Safari ya matumaini ikaendelea kwa timu hizo na hatua ya 16 bora Yanga ikakutana na TMA FC inayoshiriki Championship na kuichapa bao 1-0, huku wapinzani wake wa leo Azam FC ilicheza na Fountain Gate na kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0.

Katika hatua ya robo fainali, Yanga ikakutana na maafande wa JKT Tanzania na kikosi hicho kikashinda mabao 2-0, huku kwa upande wa Azam ikaichapa Mashujaa FC bao 1-0 na timu hizo kukata tiketi ya kucheza nusu fainali zinapokutana tena leo.

Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga, Abdihamid Moallin alisema maandalizi yote yamekamilika kwa kiwango kikubwa na wachezaji wote wako katika morali ya juu, licha ya kukiri ugumu anaoenda kukutana nao kutokana na aina ya mpinzani na ubora alionao.

“Malenho yetu ni kufanya vizuri katika mechi ya leo bila ya kuangalia siku tatu zijazo tutafanya nini dhidi yao, sio mechi rahisi kwa sababu kila tunapocheza na Azam inatupa ushindani mzuri jambo linalotupa motisha,” alisema Moallin.

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge alisema ugumu wa mechi hiyo unatokana na mahitaji ya kila timu na malengo, ingawa ushindi wa mechi sita mfululizo katika mashindano yote yanawapa hamasa wachezaji kwa ajili ya kupambana.