Ngoma imehamia Tanga

KIVUMBI cha michezo ya Ngao ya Jamii kuashiria kuanza msimu mpya wa Ligi Kuu Bara kinaanza leo katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga ambapo Simba, Yanga, Azam na Singida Fountain Gate zikiwania ngao.

Yanga ndio bingwa mtetezi wa taji hilo baada ya msimu uliopita kuichapa Simba mabao 2-1 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kwa mabao ya Fiston Mayele upande wa Yanga na bao la Simba likifungwa na Pape Sakho.

Mabingwa hao walifanikiwa kutwaa makombe yote msimu uliopita ikiwemo ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) ikiichapa Azam bao 1-0 lililofungwa na Keneth Musonda dk 13 katika mchezo wa fainali Juni 12 mwaka huu katika uwanja huo.

Ikumbukwe katika hatua ya nusu fainali Yanga ilikutana na Singida wakati Simba ikicheza na Azam na sasa ni kama vile zimebadilishana wapinzani na zinaweza kukutana kwa namna nyingine.

Endapo Yanga itaichapa Azam na Singida ikaifunga Simba au Simba akiifunga Singida na Azam ikiisambaratisha Yanga, hivyo kuzifanya timu hizo kukutana kama ilivyokuwa mchezo nusu fainali ASFC msimu uliopita.

Hata hivyo, mchezo wa Azam na Yanga ni kisasi cha aina yake kwenye uwanja huo kwa sababu Azam anarudi Mkwakwani ikiwa na kumbukumbu ya kuchapwa mchezo wa fainali zikiwa zimepita siku 53.


YANGA KIREKODI…

Tangu kuanzishwa kwa mechi za Ngao ya Jamii kwa ajili ya ufunguzi wa msimu mpya wa mashindano, Yanga ndiyo imetwaa taji hilo mara ya nyingi (saba), 2001, 2010, 2013, 2014, 2015, 2021 na 2022.

Simba imebeba mara sita 2011, 2012, 2017, 2018, 2019 na 2020, huku Mtibwa Sugar mara moja 2009 kwa kuifunga Yanga 2-1 kama ilivyokuwa kwa Azam mwaka 2016 kwa ushindi wa penalti 4-1 dhidi ya Yanga baada ya dk 90 kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Msimu uliopita Yanga ilibeba kwa kuichapa Simba mabao 2-1 na msimu wa juzi (2021), Yanga ikabeba tena kwa kuifunga Simba bao 1-0 lililofungwa na Mayele.

2020 Simba iliyokuwa abingwa wa Ligi Kuu na ASFC ilitwaa ngao kwa kuichapa Namungo mabao 2-0 yaliyofungwa na John Bocco kwa njia ya penalti na bao la pili likifungwa na Benard Morrison likiwa taji la nne mfululizo kwani ilikuwa imebeba mwaka 2017, 2018, 2019 na 2020.

Mwaka 2019, Simba iliichapa Azam mabao 4-2 huku Azam FC ikiwa ya kwanza kuandika bao kupitia kwa Shaaban Chilunda kabla ya Sharif Shiboub, kuisawazishia Simba na baadaye kuiandikia bao la pili, Clatous Chama na Francis Kahata ikamaliza kazi na bao la pili la Azam likifungwa na Frank Domayo.

Simba ilitwaa tena mwaka 2018 kwa kuichapa Mtibwa mabao 2-1, mabao yakifungwa na Meddie Kagere na Hassa Dilunga huku la Mtibwa Sugar likifungwa na Kelvin Sabato. 2017, Dabi ilipigwa ya aina yake na Simba kushinda kupitia mikwaju ya penalti 5-4 baada ya dakika 90 kumalizika kwa suluhu.

Mwaka 2012, Simba ilibeba kwa kuichapa Azam mabao 3-2 yaliyofungwa na Daniel Akkufor, Emmanuel Okwi na Mwinyi Kazimoto huku upande wa Azam yakifungwa na John Bocco na Kipre Tcheche.

Mwaka 2011 Simba ilichukua kwa mara ya kwanza kwa kuichapa Yanga 2-0 kwa mabao ya Haruna Moshi ‘Boban’ na Felix Sunzu lakini tayari Yanga ikiwa imebeba 2001 na 2010.


MAANDALIZI YALIVYO

Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Tanga (TRFA), Martine Kibua alisema maandalizi yamekamilika kwa upande wa mkoa na taratibu zote zimekaa sawa tayari kwa ajili ya michezo hiyo.

“Heshima hii tuliyopewa na TFF tunatakiwa kujivunia na niwaombe mashabiki wajitokeze katika hatua zote kuanzia siku ya kwanza hadi siku ya mwisho.”

Meneja wa Uwanjwa wa Mkwakwani, Nassoro Makau alisema walianza ukarabati wa eneo la kuchezea ‘pitch’, vyumbani, majukwaa na zoezi la mwisho lilikuwa kuweka taa kwaajili ya michezo ya usiku na tayari kila kitu kipo sawa.

“Kila kitu kimekamilika, tunachosubiri ni soka lichezwe tu,” alisema Makau.