Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ngoma akirudi tu anasaini

Muktasari:

  • Ngoma amegeuka lulu kwa kocha Fadlu Davids, tofauti na ilivyokuwa chini ya makocha Roberto Oliveira 'Robertinho' na Abdelhak Benchikha na kusababisha kuzima tetesi zote kwamba angeondoka Msimbazi.

KIKOSI cha Simba usiku wa leo kitashuka uwanjani jijini Luanda, Angola kupepetana na Bravos do Maquis, lakini taarifa njema kwa mashabiki wa klabu hiyo ni uamuzi wa mabosi wa klabu hiyo kuamua kumalizana na kiungo Fabrice Ngoma ambaye inaelezwa timu ikirudia nchini anasaini mkataba mpya.

Ngoma amegeuka lulu kwa kocha Fadlu Davids, tofauti na ilivyokuwa chini ya makocha Roberto Oliveira 'Robertinho' na Abdelhak Benchikha na kusababisha kuzima tetesi zote kwamba angeondoka Msimbazi.

Ngoma aliyetua Simba misimu miwili iliyopita akitokea Al Hilal anamaliza mkataba wake wa miaka miwili unaomalizika Juni 30, mwaka huu na mabosi wa Msimbazi wameona isiwe tabu kwa kuzungumza naye mapema ili kumuongezea na atasaini atakaporejea.

Mkongomani huyo atapewa mwaka mmoja. Tangu atue Simba amecheza chini ya makocha watatu wa kigeni ambao ni Roberto Oliveira 'Robertinho', Abdelhak Benchikha na sasa Fadlu Davids ambaye amekuwa na kismati naye kwani amerejesha makali aliyokuwa nayo awali wakati anagombewa na Simba na Yanga akiichezea Al Hilal ya Sudan.

Inaelezwa kuwa nidhamu na kujituma kwake uwanjani kumemfanya awe kipenzi cha Fadlu na kutaka aongezwe mkataba mpya kitu ambacho baada ya kuzungumza na viongozi hakuwa na hiyana ya kukubali ofa ya mwaka mmoja, lakini alitaka kwanza wamalizane na Bravos ndipo asaini mkataba mpya.

"Akitoka Angola Ngoma atasaini mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza mwaka zaidi. Kocha Fadlu amembakisha kutokana na mabadiliko yake makubwa ndani ya kikosi hicho," kilisema chanzo kutoka Simba.

Kupitia Mwanaspoti, Fadlu aliweka wazi sababu za kumpandisha cheo kiungo huyo ili kumsaidia nahodha Mohammed Hussein 'Tshabalala', ikiwamo suala la nidhamu na uzoefu alionao kulinganisha na wachezaji wengine waliopo Msimbazi kwa sasa ambao wengi ni vijana wenye damu changa.

"Ni wazi kuwa kiwango cha mchezaji huyu kimebadilika zaidi, lakini namna yake ya maisha nje na uwanja imekuwa tofauti jambo ambalo limemfanya awe kiongozi kabla hata sijamteua," alinukuliwa akisema Fadlu.

Rekodi za Ngoma msimu huu katika Ligi Kuu zinaonyesha amecheza mechi 11 akitumia dakika 757, amefunga mabao mawili huku kwenye anga za kimataifa akicheza michezo minne sawa na dakika 360.