Ngassa: Rekodi zipo ili zivunjwe

NAHODHA wa timu ya taifa, Taifa Stars, Mbwana Samatta amebakiza mabao matatu kuifikia rekodi ya Mrisho Ngassa ya mfungaji bora wa muda wote timu hiyo, huku mwenyewe akisema rekodi zipo ili zivunjwe na anasubiri kiroho safi rekodi yake ivunjwe.
Stars kesho itashuka uwanjani kumenyana na timu ya taifa ya Sudan katika mchezo wa kirafikiwa kimataifa ulio katika kalenda ya kimataifa ya FIFA utakaochezwa kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa.
Samatta amefunga mabao 22 kwenye michezo 60 akiwa na Stars, amebakiza mabao matatu kumfikia Ngassa mwenye mabao 25 anayetajwa kuwa ndio mfungaji bora wa muda wote wa Stars.
Samatta alifunga bao la ushindi kwenye pambano la kirafiki la kimataifa dhidi ya Afrika ya Kati lililoisha kwa Tanzania kushinda mabao 3-1.
Bao hilo lilikuwa la pili kwa Samatta dhidi ya Afrika ya Kati kwani bao lake la kwanza akiwa na taifa Stars alifunga dhidi ya timu hiyo mwaka 2011.
Samatta anaikaribia rekodi ya Ngassa na anaweza kuivunja kwani winga huyo wa zamani wa Yanga ameshastaafu kucheza timu ya taifa na baadaye mwaka huu kutakuwa na michezo ya kuwania kufuzu fainali za AFCON hivyo Samatta bado ana nafasi kubwa zaidi ya kuweka rekodi mpya.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ngassa alisema rekodi zinawekwa ili zivunjwe, wakati wake umeshakwisha sasa anawaachia wengine ambao bado wanaendelea kulitetea taifa kwenye kikosi cha timu hiyo.