Ngassa, Boban kuibukia Ken Gold

Sunday January 16 2022
Ngassa PIC
By Saddam Sadick

Mbeya. Baada ya kupotea Uwanjani msimu mzima, leo nyota wa zamani wa Yanga, Mrisho Ngassa anatarajia kuiongoza Ken Gold wakati timu hiyo itakapowakaribisha Pan Africa katika mchezo wa ligi ya Championship.

Mbali na Ngassa, Kiungo mkongwe pia aliyewahi kuzichezea timu kadhaa ikiwamo Simba na Yanga, Haruna Moshi Boban naye atakuwa miongoni mwa wachezaji wapya watakaoivaa Pan Africa.

Ken Gold inayoshiriki Championship, hadi sasa wapo nafasi ya tisa kwa pointi 19 ambapo watakuwa Uwanja wa Sokoine kuwakabili wapinzani hao waliopo nafasi ya 14 kwa alama 13 baada ya mechi 14 na leo itakuwa mechi yao ya mwisho kumaliza mzunguko wa kwanza.

Mkurugenzi wa timu hiyo, Keneth Mwakyusa amethibitisha wakongwe hao kuwa miongoni mwa usajili wa timu hiyo katika dirisha dogo lililofungwa usiku wa kuamkia leo Jumapili.

Amesema suala la kuanza au kutoanza litategemeana na mipango ya benchi la ufundi huku akieleza kuwa uongozi unachotaka ni mafanikio kwa klabu hiyo.

"Ni kweli ni miongoni mwa usajili wetu na leo huenda wakawepo uwanjani, ishu ya kucheza na kutocheza naiachia benchi la ufundi, sisi tunachotaka ni kuona Ken Gold inafikia malengo" amesema Mwakyusa.

Advertisement

Ken Gold huu ni msimu wake wa pili kushiriki Championship tangu walipokamilisha taratibu za kuinunua Gipco iliyokuwa na makazi yake mkoani Geita na kuihamishia wilayani Chunya mkoani Mbeya.

Advertisement