Neymar kutua Barcelona ni suala la muda tu

Muktasari:
Muda wowote huenda FC Barcelona wakafanikisha kumrejesha nyumbani Neymar kutoka PSG kutokana na mazungumzo yanayoendelea baina ya wawakilishi wa klabu hizo.
Barcelona wametuma ofa ya Paund 153milion kama ada ya kumrejesha Camp Nou nyota wao wa zamani Neymar kutoka Paris Saint-Germain huku wakijadiliana kuwa huenda Ousmane Dembele akawa sehemu ya dili hilo.
Wawakilishi wa Barcelona, akiwemo Eric Abidal na Oscar Grau, walitumia saa nne kuzungumza na mkurugenzi wa Paris Saint-Germain, Leonardo na meneja ambaye pia ni mtu kibiashara wa Jean-Claude Blanc jana mchana.
Pamoja na uwepo wa mzungumzo hayo, pande hizo mbili hazikufikia mwafaka hapo jana lakini habari njema ni kwamba kuna uwezekano wa kukutana tena na kuongea.
Neymar, 27, alijiunga na PSG akitokea Barcelona, 2017 kwa kuweka rekodi ya dunia ya Paund 200 milioni.
Mkurugenzi wa Barcelona, Javier Bordas, ambaye ni miongoni mwa wawakilishi wa timu hiyo, alithibitisha kupitia chombo kimoja cha habari nchini kwao Hispani kuwa wako mbioni kumrejesha Neymar.
“Tunakaribia kumalizana nao,” alisema Bordas akiwa uwanja wa ndege jijini Barcelona, uitwao El Prat airport.
Real Madrid nao wapo kwenye vita ya kuiwania saini ya Neymar. Wakati huo huo, PSG wanataka kumsajili Mario Mandzukic wa Juventus kutokana na kuumia kwa Edinson Cavani na Kylian Mbappe.