Ndumbaro: Mashabiki wanaopokea wageni kushughulikiwa

WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Damas Ndumbaro amesema Serikali itakutanma na Shirikisho la Soka nchini na klabu za Simba na Yanga ili kuona inatoa mchango gani kuhakikisha timu hizo zinafanya vizuri robo fainali na kusonga mbele.

Waziri Ndumbaro amesema pamoja na mambo mengine, amewataka mashabiki kuacha kuwapokea mashabiki na wafahamu mechi hizi za robo fainali ni kufa na kupona na kinachotakiwa ni kuhakikisha timu zetu zinashinda.

Amesema Serikali itakula sahani moja na mashabiki wa Simba na Yanga ambao wataenda kupokea wageni uwanja wa ndege na kuwasapoti.

"Wiki iliyopita tulitoa tamko, Serikali tunataka kukaa na Simba, Yanga na TFF, ili watuambie kama serikali, tunahitaji kutoa mchango gani ili timu kushinda robo fainali na ziingie nusu fainali. Tunaweza kukutana Jumanne wiki ijayo ili kupanga mikakati."

Kuhusu mashabiki amesema; "Watanzania niwaombe sana najua kuna utani wa jadi, lakini kwenye mechi hizi za robo fainali ni mechi za kufa na kupona, hatutegemei kuona Mtanzania yeyote akienda kupokea wageni uwanja wa ndege, ama kuvaa jezi za timu za wageni."

"Sisi kama Serikali hatutawaachia hili TFF wala Simba na Yanga, kwa hiyo tukihangaika na mtu ambaye tutaona ni msaliti. Tunaomba Watanzania watuelewe na watusamehe kwa sababu tunataka timu hizi zifanikiwe."

"Kwa hiyo wewe Mtanzania ambaye utaweka kimbelembele kwenda kupokea wageni uwanjani wa ndege, kuwasapoti kwa namna yeyote, hatutakuelewa na tutadili na wewe kwa vile ambavyo tunaona inafaa."

"Tumekuwa nchi pekee iliyofanikiwa kuingiza timu mbili mwaka huu, lakini ukishapata mafanikio haupaswi kutumia muda mwingi sana kushangilia hayo mafanikio, unatakiwa uangalie unafanya nini ili kuendelea kupata mafanikio zaidi."

Amesema hayo leo Machi 13, 2024 wakati akichangia mjadala wa Mwananchi Space, uliandaliwa na Mwananchi Communications Ltd, wenye mada isemayo 'Ipi nafasi ya Simba, Yanga kwenye vita ya kusaka nusu fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.