Ndumbaro alamba cheo TFF

Dar es Salaam. Wakati msimu mpya wa mashindano yanayosimamiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ukitarajiwa kuanza mwezi huu Kamati ya utendaji ya shirikisho hilo imeteua Kamati ya Rufaa ya leseni za klabu huku Wakili Dk.Damas Ndumbaro akiteuliwa kuwa mwenyekiti.

Ndumbaro alifungiwa kujihusisha na soka kwa miaka saba kabla ya kufutiwa adhabu na kamati ya nidhamu ya TFF hivi karibuni.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TFF kwa vyombo vya habari Wakili Alex Mgongolwa ameteuliwa kuwa makamu mwenyekiti wakati wajumbe wa kamati hiyo ni Charles Matoke, Tumainiel Mlango na Ahmed Menye.

Kwa mujibu wa kanuni za uendeshaji wa mashindanoi yanayosimamiwa na TFF, kamati hiyo itakuwa na jukumu la kuhakikisha klabu za Ligi Kuu zinakidhi vigezo na masharti ya msingi kabla ya kupatiwa leseni za kushiriki Ligi Kuu.

"Leseni inataka klabu kuwa na uwanja wa mazoezi, timu ya vijana, uwepo wa ofisi rasmi na watendaji wake akiwemo mtendaji mkuu, maofisa masoko, habari na mhasibu mwenye taaluma ya uhasibu," imesema taarifa hiyo.

Wakati huohuo, Ligi Daraja la Kwanza (FDL) imepangwa kuanza Septemba 16 ikishirikisha timu 24 zilizogawanywa kwenye makundi matatu yenye timu nane kila moja.