Ndemla kuwakosa Mbeya City

Muktasari:

  • Timu hiyo imeweka kambi kwa siku nane (8) Jijini Dodoma kujiandaa na mchezo huo pamoja na michezo ya Ligi Kuu Bara.
  • Mratibu wa timu hiyo, Ibrahim Mohammed alisema sababu ya Ndemla  kuukosa mchezo huo ni kutokana na kuwa na kadi tatu za njano.

DODOMA. KIUNGO wa Singida Big Stars, Said Ndemla anatarajia kuukosa mchezo wa robo fainali ya Kombe la Azam Sports Federation (ASFC) dhidi ya Mbeya City unaotarajiwa kufanyika Aprili  2 mwaka huu katika uwanja wa Liti mkoani Singida.

Timu hiyo imeweka kambi kwa siku nane (8) Jijini Dodoma kujiandaa na mchezo huo pamoja na michezo ya Ligi Kuu Bara.
Mratibu wa timu hiyo, Ibrahim Mohammed alisema sababu ya Ndemla  kuukosa mchezo huo ni kutokana na kuwa na kadi tatu za njano.

Kuhusu kambi ya timu hiyo Jijini Dodoma,Mratibu huyo alisema : “Tumeamua kuweka kambi Dodoma kutokana na hali za hewa ya Dodoma kuwa sawa na Singida na tutakuwa hapa kwa siku nane kisha tutarejea Singida kucheza dhidi ya Mbeya City,”.

Alisema kambi hiyo itawakosa wachezaji watatu,Meddie Kagere ambaye yupo na timu ya Taifa ya Rwanda na Yusuphu Kagoma  na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ na Kelvin Nashon ambaye aliumia  katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union katika uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.

Katika hatua nyingine Chama  cha Soka Mkoa wa Singida (Sirefa) kimesema mkataba ilioingia Singida Big Stars na Klabu ya US Monastir ya Tunisia ni fursa kubwa kwao hasa katika soka la vijana.

Machi 20 mwaka huu  klabu ya SBS ilisaini mkataba wa mashirikiano na klabu ya US  Monastir ya nchini Tunisia kwa lengo la kushirikiana katika maendeleo mbalimbali  ya kimkakati.
Maeneo watakayoshirikiana ni pamoja na kubadilishana ujuzi na uzoefu wa kitaaluma,usajili wa wachezaji,eneo la ufundi pamoja na kuendeleza timu za vijana kupitia akademi ya Monastir.

Mwenyekiti wa Sirefa Hamis Kitila aliupongeza uongozi wa SBS kwa kuitafuta fursa hiyo na kudai soka la Singida kila siku limekuwa likipiga hatua kupitia timu hiyo.

“Tunajivua uwepo wa SBS kwetu mkataba ule ni mkubwa, kwetu sisi tuna timu ya vijana na kuna baadhi wanatoka hapa kwetu tunaamini ndio wakati mzuri wa kuzidi kujitangaza vijana wetu,”alisema Kitila.