Ndemla aandaliwa programu

Tuesday September 14 2021
ndemla pic
By Olipa Assa

NI kama Said Ndemla amepeleka matumaini Mtibwa Sugar, baada ya wachezaji wa timu hiyo kusubiri kwa hamu mguu wake kufanya maajabu itakapoanza Ligi Kuu Bara, Septemba 29.
Ndemla amejiunga na Mtibwa Sugar akitokea Simba iliyomlea tangu akiwa kikosi B, jambo lililoonekana kuwafurahisha wengi kuona atakiokoa kipaji chake.
Meneja wa Mtibwa Sugar, David Bgoya alisema kati ya usajili walioufanya msimu huu ambao umeonekana kuwafurahisha mashabiki wao ni pamoja na Ndemla wanayemuona ataonyesha ufundi wake.
“Msimu huu Mtibwa Sugar tumesajili wachezaji wengi wazuri akiwemo Ndemla, Abdi Banda, Ibrahim Ame na wengine wengi. Hii inatupa picha ya namna tutakavyoachana na maumivu ya misimu miwili nyuma tuliyoponea chupuchupu kushuka,” alisema.
Nahodha wa timu hiyo, Dickson Daud alisema Ndemla ni kama kiongozi kwake akikaa naye kumjenga kuhusu mazingira mapya ya kufanya kazi.
“Naelewa wachezaji wanaotoka Simba na Yanga wanapokwenda kujiunga na timu nyingine wanapotea kwa kuwa wanaona ndio mwisho wao, nimefurahia sana kumuona Ndemla ambaye nitakuwa na kikao naye,” alisema Daud.
“Nitakipigania kipaji chake hadi kuhakikisha anakuwa mchezaji ghali, nilichelewa kuingia kambini, ila nitamjenga kwamba aanze moja, kwani ni kati ya wachezaji ambao nawakubali sana, nimefurahi sana kumuona kwenye timu yangu,” alisema.
Daud alisema Ndemla hana haja ya kuwaangalia mashabiki wanasemaje, badala yake awajibu kwa mguu wake ambao una madini ambayo hayajatumika, kutokana na kukosa nafasi ya kucheza Simba.
“Atulize akili tu, atakuwa mfano wa kuigwa na wengine, akipata mechi nyingi Ndemla ni dhahabu na Mtibwa Sugar ni sehemu sahihi sana kwake, maana tunaishi kama familia,” alisema.
Kwa upande Salum Kihimbwa naye alifurahishwa na Ndemla kuwa Mtibwa Sugar akiamini kwamba kipaji chake kitakwenda kuwastajabisha wengi.
“Jamaa ana kipaji kikubwa, kama atajituma atakuwa habari nyingine na haya maneno yangu ipo siku yataishi,” alisema.
Mtibwa Sugar imewasajili Abdi Banda (huru), Ibrahim Ame na Said Ndemla (Simba), Styve Nzigamasabo (Namungo FC) na Issac Kachwele. Waliotoka ni Hassan Kessy, Ismail Aidan na Haruna Chanongo.
Katika Ligi Kuu Bara timu inatarajiwa kuanza michuano hiyo kwa kumenyana na Mbeya Kwanza, Septemba 27 katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Advertisement